Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha sementi cha Dangote cha Mtwara Aliko Dangote wa Nigeria Kushoto na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) Bw. Gilead John Teri  kulia wakati alipokutana nao kwa mazungumzo ikulu jijini Dar es Salaam Mei 16, 2026.

…………. 

Na John Buluku, Dar es Salaam

Katika kipindi hiki ambacho mataifa mengi duniani yanapambana kujenga uchumi kupitia uwekezaji mkubwa, Tanzania imeendelea kujijengea nafasi ya kipekee chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kutumia diplomasia ya uchumi inayolenga ushirikiano, utulivu na kujenga mazingira bora ya biashara.

Ndiyo maana katika siku za hivi karibuni, mjadala uliofanyika Nairobi kuhusu uwekezaji wa mradi mkubwa wa kusafisha mafuta ghafi (refinery) unaodaiwa kutaka kujengwa Tanga ulivuta hisia za Watanzania wengi. Katika jukwaa hilo walionekana Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Kenya William Ruto pamoja na mfanyabiashara mkubwa wa Afrika Aliko Dangote wakijadili mustakabali wa mradi huo wa kimkakati kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa Mtanzania wa kawaida, ilikuwa rahisi kujiuliza kwa nini Tanzania haikuonekana wazi katika jukwaa hilo wakati eneo linalotajwa kuhusishwa na mradi huo liko ndani ya mipaka ya Tanzania. Hata hivyo, ni muhimu pia kutambua kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya Serikali ya Tanzania iliyothibitisha rasmi utekelezaji wa mradi huo mkoani Tanga. Hivyo, mjadala uliokuwa ukiendelea Nairobi ulionekana zaidi kuwa sehemu ya maono na mazungumzo ya wawekezaji pamoja na wadau wa kikanda kuhusu uwezekano wa mradi huo katika siku zijazo.

Taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu, imeweka picha pana zaidi kuhusu namna Serikali ya Tanzania ilivyo tayari na inavyosimamia kwa umakini diplomasia ya uchumi. Kupitia taarifa hiyo, imeelezwa kuwa Aliko Dangote amekutana na kuzungumza na Samia Suluhu Hassan Ikulu Dar es Salaam na kujadili maeneo mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo nishati, viwanda, bandari, gesi, mbolea pamoja na uwezekano wa kuingia ubia katika mradi wa kusafisha mafuta ghafi unaokadiriwa kugharimu dola bilioni 17 za Marekani.

Hapa ndipo nguvu ya diplomasia ya uchumi ya Rais Dkt. Samia inapodhihirika. Serikali imeendelea kutumia njia ya mazungumzo ya moja kwa moja, kujenga imani kwa wawekezaji na kuhakikisha kuwa kila hatua ya uwekezaji mkubwa inafanyika kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa. Hii ndiyo sababu hata katika mazingira ya mijadala ya kikanda, Tanzania imeendelea kubaki kuwa sehemu muhimu ya maamuzi kutokana na utulivu wake wa kisiasa na sera zake rafiki kwa uwekezaji.

Kauli za Aliko Dangote mwenyewe zinaonesha mabadiliko makubwa ya mazingira ya biashara nchini. Alipompongeza Rais Samia kwa kushughulikia changamoto zilizokuwa zinaikabili kampuni yake ya saruji Mtwara, aliweka wazi kuwa Tanzania imeendelea kuwa eneo muhimu la kimkakati kwa uwekezaji wake barani Afrika. Hii ni ishara kuwa diplomasia ya uchumi inayotekelezwa sasa inaleta matokeo yanayoonekana kwa wawekezaji wakubwa wa kimataifa.

Aidha, hatua ya Dangote Group kuleta malori 400 yanayotumia gesi asilia nchini inaonesha namna wawekezaji wanavyoendelea kuwa na imani na sera za nishati safi pamoja na mazingira bora ya biashara nchini Tanzania. Haya ni matokeo ya maamuzi ya kimkakati yanayolenga kuvutia uwekezaji wenye tija kwa Taifa.

Katika mazingira hayo, mjadala wa refinery unaodaiwa kutaka kujengwa Tanga unapaswa kuonekana kama fursa nyingine ya Tanzania kuendelea kujijengea nafasi kubwa zaidi katika uchumi wa kikanda. Miradi mikubwa ya aina hii huhitaji majadiliano marefu, ushirikiano wa nchi mbalimbali na makubaliano ya kina kabla ya kufikia hatua ya utekelezaji rasmi. Ndiyo maana taarifa rasmi kutoka serikalini huwa na umuhimu mkubwa katika kutoa mwelekeo halisi wa jambo husika.

Kwa mtazamo wa wengi, jambo muhimu zaidi si nani alikaa kwenye jukwaa la kwanza Nairobi, bali ni namna Tanzania inavyoendelea kujenga mazingira yatakayowezesha miradi mikubwa ya kimkakati kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi wake. Hapo ndipo uongozi wa Samia Suluhu Hassan umeendelea kuonekana ukitanguliza utulivu, mazungumzo na ushirikiano wa kiuchumi badala ya mihemko ya kisiasa.

Kauli ya Rais Dkt. Samia ya kumhakikishia Aliko Dangote ushirikiano na kumkaribisha kuendelea kuangalia fursa zaidi za biashara na uwekezaji nchini ni ishara nyingine ya namna Tanzania ilivyoamua kufungua milango kwa uwekezaji wenye manufaa mapana kwa Taifa. Aidha, mwaliko wa Rais kwa Dangote Group kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea unaonesha mtazamo mpana wa serikali katika kuimarisha sekta za kimkakati zinazogusa moja kwa moja uchumi wa wananchi, hususan kilimo ambacho kinaajiri mamilioni ya Watanzania.

Hii inaonesha kuwa diplomasia ya uchumi ya Tanzania haijikiti tu kwenye miradi mikubwa ya nishati na viwanda, bali pia inalenga kuongeza uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kufungua fursa mpya za ajira pamoja na ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Mwisho, tukio hili limetoa funzo muhimu kuhusu namna diplomasia ya uchumi inavyofanyika katika dunia ya sasa. Tanzania imeendelea kuonesha kuwa ipo tayari kushirikiana na wawekezaji wakubwa na mataifa ya ukanda kwa maslahi mapana ya maendeleo ya uchumi, huku ikiendelea kulinda hadhi na maslahi ya Taifa kupitia maamuzi yenye busara na utulivu mkubwa wa kiuongozi.