Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani katika makao makuu wa shirika hilo jengo la International Dar es Salaam. 

…………….

Kampuni ya Puma Energy Tanzania imetangaza kuzindua rasmi programu ya kidijitali ya PRIS yenye lengo la kuwazawadia wateja kupitia manunuzi ya mafuta, vilainishi pamoja na bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika vituo vyake nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mei 13, 2026 wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafunzo ya matumizi ya programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah alisema uzinduzi wa PRIS App ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuendana na mwelekeo wa uchumi wa kidijitali nchini.

“Puma Energy Tanzania inaunga mkono Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Dijitali Tanzania (2024–2034), unaolenga kuiweka nchi kama kitovu cha kidijitali cha kikanda kwa kuimarisha miundombinu, kupanua ujumuishaji wa kifedha na kuendesha ukuaji wa uchumi,” alisema Bi. Abdallah.

Alisema programu hiyo itawapa wateja fursa ya kupata zawadi mbalimbali kila wanapofanya manunuzi katika vituo vya Puma Energy, ikiwa ni njia ya kuwarudishia thamani kwa kuendelea kutumia huduma za kampuni hiyo.

Bi. Abdallah alieleza kuwa Puma Energy inaendesha zaidi ya vituo 2,201 vya rejareja na kuhudumia viwanja vya ndege 107 duniani kote, huku ikilenga kuongeza uwekezaji wake zaidi ifikapo mwaka 2030 ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, alisema kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kwa Serikali kupitia kodi na ushuru mbalimbali. Pia mwaka 2025 kampuni hiyo ilitangaza gawio la shilingi bilioni 21 kutokana na umiliki wa Serikali wa asilimia 50 kupitia Msajili wa Hazina.

“Mafanikio ya uzinduzi wa PRIS katika nchi za Zimbabwe, Malawi na Botswana yameonesha mwitikio mkubwa wa wateja, na sasa Tanzania inakuwa soko la nne barani Afrika kuzindua huduma hii,” alisema.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kampuni hiyo inatoa huduma ya mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege nane nchini, ikiwemo viwanja vitatu vya kimataifa na vingine vya ndani. Aidha, amewatoa hofu wadau wa sekta ya usafiri wa anga kwa kusema kampuni hiyo ina akiba ya kutosha ya mafuta ya ndege na inaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka mbalimbali za Serikali zinazohusika na uagizaji wa mafuta nchini.

“Tuna mafuta ya ndege ya kutosha na tuna mawasiliano mazuri na mamlaka zote zinazohusika katika uagizaji wa mafuta, hivyo wadau wa viwanja vya ndege na wateja wetu waendelee kuwa na imani nasi kwani tutaendelea kutoa huduma bila shaka yoyote,” alisema Bi. Abdallah.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani katika makao makuu wa shirika hilo jengo la International Dar es Salaam. kushoto ni Bi. Lilian Kanora, Meneja Masoko Puma Energy Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah akizungumza na waandishi wa habari kushoto akimsikiliza Bw. Sulpis Mmasi, Meneja Mauzo ya Rejareja Puma Energy Tanzania wakati akifafanua baadhi ya