Na Happy Lazaro, Arusha 
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa tathmini ya utendaji kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mkoani Arusha, ukilenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa walipa kodi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Mwenda, amesema mamlaka hiyo itaendelea kusimamia ukusanyaji wa kodi kwa haki, heshima na weledi, huku ikiongeza jitihada za kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari. 
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanategemea kujenga imani ya walipa kodi pamoja na kuhakikisha wananchi wanaona matokeo ya kodi zao kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mwenda amesema TRA itaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kikodi kwa kutumia mifumo ya kisasa ili kurahisisha ulipaji wa kodi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na walipa kodi wote nchini.
Amebainisha kuwa tangu Rais  Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, makusanyo ya kodi yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka takribani shilingi trilioni 21 kwa mwaka hadi kufikia shilingi trilioni 37.9, hali inayodhihirisha kuimarika kwa usimamizi wa mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa TRA, Moshi Kabengwe, amesema mkutano huo wa siku tano unawakutanisha washiriki 477 kutoka ndani ya mamlaka hiyo pamoja na wadau mbalimbali.
 Ameeleza kuwa TRA imefanikiwa kuweka rekodi ya kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa miezi 12 mfululizo, ikiwa na wastani wa asilimia 105.24 katika mwaka wa fedha 2025/2026, na sasa inalenga kukusanya takribani shilingi trilioni 41 katika mwaka ujao wa fedha.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Kilenga Swai, amesema ushirikiano uliopo kati ya TRA na wafanyabiashara umeendelea kuimarika na kusaidia kujenga mazingira bora ya biashara. 
Hata hivyo, ameiomba TRA kuboresha mfumo wa service levy ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Arusha, Ahmed Jamali, ameiomba TRA kushirikiana na mamlaka nyingine kutafuta suluhisho la changamoto ya wajasiriamali wadogo wanaofanyia biashara mbele ya maduka, akisema hali hiyo imekuwa ikiathiri wafanyabiashara wanaolipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Washiriki wa mkutano huo pia waliipongeza TRA kwa kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, wakieleza kuwa imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa. 
Wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, kurahisisha taratibu za kikodi na kuongeza elimu kwa walipa kodi ili kuongeza utii wa hiari na mapato ya Serikali.