Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Glory Mtui akichukua sampuli ya damu ya Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha Lucius Mwenda wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya kwa watumishi wa wizara hiyo iliyomalizika jana katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Fedha jijini Dodoma.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) John Mirisho akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali wa Wizara ya Fedha, Chotto Sendo wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya kwa watumishi wa wizara hiyo iliyomalizika jana  jijini Dodoma.

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha wakisubiri kupata huduma za uchunguzi wa afya zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya iliyomalizika jana jijini Dodoma.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moris Budotela  akitoa elimu ya “Jua Namba Zako” kwa Afisa Sheria wa Idara ya Huduma za Sheria wa Wizara ya Fedha Yohana Msengi  wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya iliyomalizika jana jijini Dodoma.

 Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce  akitoa elimu ya “Jua Namba Zako” kwa mtumishi wa Wizara ya Fedha wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya kwa watumishi hao iliyomalizika jana jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akitoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa mfanyakazi wa Wizara ya Fedha wakati wa kambi maalumu ya upimaji wa afya kwa watumishi hao iliyomalizika jana jijini Dodoma. (Picha na JKCI)

…………

Na Mwandishi Maalumu – Dodoma

15/5/2026 Jumla ya watumishi 441 wa Wizara ya Fedha wamepata huduma za uchunguzi wa afya ya moyo katika kambi maalumu ya siku tano iliyomalizika jana katika wizara hiyo jijini Dodoma kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

Kambi hiyo iliratibiwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo Dkt. Kisenge alisema lengo la kambi hiyo ilikuwa ni kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo karibu zaidi na wananchi pamoja na kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

“Magonjwa ya moyo hususan shinikizo la juu la damu  ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vya watu wengi duniani. Kutokana na hali hiyo tumeona ni muhimu kutoa elimu ili wananchi waone umuhimu wa kupima afya zao, kutambua hali zao mapema na kuchukua hatua kabla hawajapata matatizo makubwa ya kiafya”.

“Kati ya watu tuliowaona 76 walibainika kuwa na shinikizo la juu la damu, 18 walikutwa na tatizo la kisukari, 60 walikuwa na kiwango kikubwa cha mafuta mwilini huku 33 wakipewa rufaa ya kuja JKCI kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi”, alisema Dkt. Kisenge. . Aidha, watu 123 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi

Dkt. Kisenge alisema baadhi ya watu waliokutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu hawakuwa wanajijua kabisa kuwa na shida hiyo, mmoja alikutwa na tatizo la kutanuka kwa kuta za moyo na mmojatatizo la kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo nao hawa hawakuwa wanajijua kuwa na shida hizo.

“Kati ya watu tuliowaona kuna ambao walikuwa na changamoto ya shinikizo la juu la damu. Wachache walikuwa tayari wanajua hali zao lakini wengine walikuwa hawajui kabisa na kwa baadhi yao tumewaanzishia matibabu” alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka ili waweze kutambua hali zao mapema na kuchukua hatua stahiki kabla magonjwa hayajawa makubwa.

Kwa upande wao  watumishi wa Wizara ya Fedha waliopata huduma hizo waliishukuru JKCI kwa kuwafikishia huduma ya upimaji wa moyo  karibu na maeneo yao ya kazi huku wakisema zimewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata elimu muhimu ya namna ya kuishi maisha yenye afya.

John Nicodem ambaye ni Mhasibu Mwandamizi wa Wizara ya Fedha alisema huduma hizo zimemwezesha kupata tathmini ya afya yake pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kuendelea kuishi kwa afya bora.

“Nimefurahi kupata huduma hizi kwa sababu zimenisaidia kujua hali yangu ya afya. Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kupima afya mara kwa mara lakini ni jambo muhimu sana ili tujue hali zetu mapema na kupata ushauri wa kitaalamu”,  alisema John.

Naye Neema Nyipamato Msaidizi wa Usimamizi wa Kumbukumbu alisema elimu ya maogonjwa ya moyo aliyoipata imemsaidia kutambua umuhimu wa kuanza mapema kujenga msingi wa maisha bora ya afya.

“Nimejifunza umuhimu wa kula lishe bora, kufanya mazoezi na kujenga mtindo mzuri wa maisha tangu ukiwa kijana. Afya bora ya uzeeni inaanza na maamuzi tunayofanya leo” alisema Neema.