Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

Serikali imenunua na kusimika vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu vyenye thamani ya Shilingi bilioni 241.6 katika hospitali mbalimbali nchini.

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa vifaa hivyo vinapatikana kuanzia ngazi ya hospitali ya Taifa hadi vituo vya afya ya msingi.

‎Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo , Mei 11, 2026,  bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amebainisha kuwa idadi ya mashine za MRI imeongezeka kutoka saba hadi 13 huku CT Scan zikiongezeka kutoka 12 hadi 45.

Pia ameongeza kuwa Serikali imefanikiwa kupata huduma ya PET CT SCAN ambayo haikuwepo awali nchini pamoja na kuongeza vifaa vya Digital X-Ray na Ultrasound. 

Amesema kuwa ongezeko la vifaa hivyo limepunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi pamoja na kusaidia wananchi kupata matibabu kwa gharama nafuu.

Aidha amesema kuwa uwezo wa kugundua magonjwa umeongezeka kufuatia uwekezaji mklubwa uliofanywa katika sekta ya afya nchini.