Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametambuliwa kuwa kinara wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika Bara la Afrika kufuatia mafanikio yaliyopatikana nchini katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Waziri wa Afya , Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika huduma za afya pamoja na dhamira ya kupunguza vifo vya kina mama wajawazito.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo , Mei 11, 2026, bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amebainisha kuwa Serikali imejipanga kupunguza kwa asilimia 50 vifo vitokanavyo na uzazi ifikapo mwaka 2030.
Pia ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuvuka malengo ya maendeleo endelevu ya dunia yanayotaka vifo vitokanavyo na uzazi viwe chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Amesema kuwa Rais Samia ameendelea kutambuliwa kama kiongozi aliyefanya vizuri kwa muda mfupi katika kuboresha huduma za afya nchini.
Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika afya ya uzazi, mama na mtoto ili kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha wakati wa kujifungua.
