‎Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

‎Wizara ya Afya imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,800,262,058,000 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta ya afya nchini.

‎Fedha hizo zinajumuisha Shilingi 637,444,765,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na Shilingi 1,162,817,293,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

‎Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya hadi hospitali za rufaa na Taifa.

‎Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, huduma za chanjo pamoja na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

‎Pia ameongeza kuwa sehemu ya fedha hizo zitatumika kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya afya, kuongeza wataalamu wa afya pamoja na kuimarisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi nchini.

‎Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wakati kupitia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika sekta ya afya nchini.