Na John Bukuku
Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Tanzania hadi Mombasa nchini Kenya unatajwa kuongeza hamasa mpya ya upekee wa uhusiano na ushirikiano wa Wakenya na Watanzania huku mataifa hayo mawili yakizidi kuimarisha mshikamano wa kihistoria uliodumu kwa miongo mingi kupitia biashara, mwingiliano wa makabila, tamaduni pamoja na diplomasia ya uchumi ndani ya Afrika Mashariki.
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto nchini Tanzania imeendelea kudhihirisha namna ambavyo diplomasia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyozidi kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kijamii na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Tofauti na mahusiano mengi ya kidiplomasia yanayojengwa kwa mikataba ya kisiasa pekee, Tanzania na Kenya zimeendelea kuunganishwa na jamii zinazopatikana pande zote mbili za mipaka yao ikiwemo Wamaasai, Wakurya, Wajaluo na baadhi ya koo za Wachaga, hali inayofanya wananchi wa nchi hizo kujiona kama familia moja yenye historia na tamaduni zinazofanana.

Kwa mfano, jamii ya Wamaasai imeendelea kuishi katika maeneo ya Kaskazini mwa Tanzania na Kusini mwa Kenya huku ikidumisha mshikamano wa kitamaduni na kijamii bila kujali mipaka ya kisiasa. Vivyo hivyo kwa Wakurya wanaopatikana Mkoa wa Mara nchini Tanzania na upande wa Kenya karibu na mpaka wa Sirari ambapo wameendelea kushirikiana katika biashara, ufugaji na shughuli nyingine za kijamii.
Aidha, Wajaluo wameendelea kuwa sehemu muhimu ya mwingiliano wa wananchi wa nchi hizo mbili kupitia shughuli za biashara, elimu, ajira pamoja na ndoa za kijamii zinazounganisha familia kutoka Tanzania na Kenya. Pia baadhi ya koo za Wachaga zimekuwa zikihusishwa na historia ya mwingiliano wa wananchi wa maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro kati ya Tanzania na Kenya.
Mbali na muingiliano wa makabila, lugha ya Kiswahili imeendelea kuwa nyenzo kubwa ya kuimarisha ushirikiano huo. Tanzania na Kenya zimekuwa mataifa muhimu katika kukuza matumizi ya Kiswahili ndani ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla, jambo ambalo limeongeza urahisi wa biashara na mawasiliano kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
Ziara ya Rais William Ruto nchini Tanzania imekuja katika kipindi ambacho diplomasia ya uchumi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuifungua Tanzania katika nyanja za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeendelea kujijengea ushawishi mkubwa wa kidiplomasia kupitia sera za ushirikiano na majirani zake wa Afrika Mashariki.
Kwa muda mrefu wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya wamekuwa wakitegemeana katika biashara ya bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula, vifaa vya ujenzi, bidhaa za viwandani pamoja na huduma za usafirishaji. Ushirikiano huo umechangia kuongeza ajira, mapato ya serikali pamoja na ukuaji wa uchumi wa mataifa hayo mawili.
Miongoni mwa bidhaa zinazouzwa kwa wingi nchini Kenya kutoka Tanzania ni vyakula mbalimbali pamoja na mbao kutoka Mufindi mkoani Iringa ambazo zimeendelea kuwa bidhaa muhimu katika sekta ya ujenzi na viwanda nchini humo. Hii inaonesha namna ambavyo rasilimali za Tanzania zimeendelea kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Afrika Mashariki.
Kadhalika, Kenya imeendelea kuwa soko muhimu kwa bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania huku wawekezaji wa Kenya wakiongeza uwekezaji katika sekta za huduma, usafirishaji, teknolojia pamoja na viwanda nchini Tanzania. Ushirikiano huo umeendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Hatua kubwa zaidi iliyojitokeza katika ziara ya Rais Ruto ni makubaliano ya ushirikiano wa sekta ya nishati hususan mradi wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa. Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayobadili sura ya biashara ya nishati katika Afrika Mashariki.
Kupitia mradi huo, Tanzania itanufaika kwa kupanua soko la gesi asilia wakati Kenya itanufaika kwa kupata nishati ya uhakika kwa matumizi ya viwanda na uzalishaji wa umeme. Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa mradi huo unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa kikanda katika miaka ijayo.
Kwa mtazamo wa diplomasia ya uchumi, makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wenye manufaa makubwa kwa mataifa yote mawili. Mbali na kuongeza biashara, mradi huo unaweza kusaidia kuvutia uwekezaji mkubwa wa viwanda, kuongeza ajira na kuifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu muhimu cha biashara ya nishati barani Afrika.
Mbali na sekta ya nishati, Tanzania na Kenya pia zilisaini mikataba mingine katika maeneo ya reli, usafiri wa majini, kilimo, viwango vya bidhaa pamoja na ushirikiano katika utumishi wa umma. Mikataba hiyo imeonesha dhamira ya viongozi hao wawili katika kuimarisha maendeleo ya pamoja ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika mazungumzo yao, Rais Samia na Rais Ruto walisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa changamoto kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya. Kauli hiyo imepokelewa vizuri na sekta binafsi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikilalamikia urasimu katika mipaka ya nchi hizo mbili.
Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Rais Ruto alisema kuwa Afrika Mashariki haiwezi kufikia maendeleo ya kweli bila kuwepo sera zinazorahisisha biashara, uwekezaji na usafiri wa watu ndani ya ukanda huo. Hotuba yake ilionesha msukumo mpya wa kuifanya EAC kuwa jumuiya yenye nguvu zaidi kiuchumi.
Rais Ruto pia alieleza kuwa wananchi wa Afrika Mashariki tayari wameunganishwa kiasili kupitia biashara, historia na tamaduni zinazofanana, hivyo jukumu la viongozi ni kuweka mazingira bora yatakayorahisisha ushirikiano huo badala ya kuweka vikwazo vya kiutawala.
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mhe. Bakari Shingo, amesema kuwa ushirikiano wa Tanzania na Kenya una manufaa makubwa kwa wananchi wa kawaida hasa wafanyabiashara wadogo wanaotegemea soko la kikanda katika kukuza uchumi wao. Amesema kuwa Afrika Mashariki inahitaji utekelezaji wa vitendo ili wananchi waweze kuona faida halisi za umoja huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Butiama, Mhe. Dkt. Wilson Mahera, amesema kuwa hotuba ya Rais Ruto imebeba maono yanayofanana na falsafa ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuhusu umuhimu wa mshikamano wa Afrika.
Amesema kuwa umoja wa kiuchumi wa Tanzania, Kenya na Uganda unaweza kuwa msingi mkubwa wa kupunguza umaskini, kuongeza ajira kwa vijana na kuifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu cha maendeleo barani Afrika.
Dkt. Mahera ameongeza kuwa ujio wa viongozi mbalimbali wa Afrika Mashariki nchini Tanzania unaonesha namna ambavyo uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeendelea kuijenga Tanzania kama kitovu cha diplomasia ya Uchumi kikanda.
Amesema kuwa ushirikiano huo ukisimamiwa vizuri unaweza kuongeza biashara, kuimarisha amani na kufungua fursa mpya za uwekezaji kwa wananchi wa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Kwa ujumla, ziara ya Rais William Samoei Ruto nchini Tanzania imeonesha wazi kuwa diplomasia ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuijenga Tanzania kama nguzo muhimu ya mshikamano wa Afrika Mashariki.
