Na John Bukuku, Dar es Salaam
Ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Rwanda umeendelea kuimarika kwa kasi katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, ukichochewa na sera ya Diplomasia ya Uchumi inayolenga kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kuimarisha miundombinu ya kikanda.
Katika muktadha huo, ushawishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika diplomasia ya uchumi umeendelea kujidhihirisha kwa kasi kubwa kupitia kuongezeka kwa mikutano ya kikanda na kimataifa inayofanyika nchini, pamoja na uimarishaji wa mahusiano ya kibiashara na mataifa jirani. Serikali yake imeweka msukumo mpya katika kufungua Tanzania kiuchumi, ambapo uwekezaji na biashara vinapewa kipaumbele kama nyenzo kuu ya mahusiano ya kimataifa.
Aidha, diplomasia hiyo ya kiuchumi imeiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha majadiliano ya kikanda, ambapo mikutano ya viongozi na makongamano ya kimataifa yamekuwa yakifanyika mara kwa mara nchini. Hali hii imeongeza imani ya wawekezaji na washirika wa maendeleo, huku ikiiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati kama daraja la biashara na ushirikiano ndani ya Afrika Mashariki.
Mchambuzi wa siasa na uchumi, Thomas Joel Kibwana, amesema ushawishi wa Rais Samia Suluhu Hassan, umeendelea kuimarika katika ukanda wa Afrika Mashariki, hali inayodhihirika kupitia ziara za viongozi wakuu wa mataifa jirani pamoja na ongezeko la mikutano ya kimataifa inayofanyika nchini.
Amesema miongoni mwa viashiria hivyo ni ziara za hivi karibuni za Rais wa Rwanda, Paul Kagame, pamoja na Rais wa Kenya, William Samoei Ruto, ambazo zinaonesha namna Tanzania ilivyofungua milango yake kwa dunia na kuwa kitovu cha majadiliano ya kikanda na kimataifa, akisisitiza kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinategemeana kiusalama, kiuchumi na kisiasa.
Aidha, Kibwana ameeleza kuwa ongezeko la makongamano ya kimataifa, ikiwemo mikutano ya kitaaluma kama ya wanasheria wa Afrika Mashariki, linaashiria kuimarika kwa nafasi ya Tanzania kama eneo la kuvutia viongozi wa kisiasa, sekta binafsi na taasisi mbalimbali kujadili masuala ya maendeleo, ambapo takwimu za biashara zinaendelea kuonesha mwelekeo chanya.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Abed, kuanzia mwaka 2021 shehena ya mizigo imeongezeka kutoka tani 1,253,335 hadi kufikia tani milioni 1,668,602, hali inayoonesha mafanikio makubwa ya usimamizi wa bandari na kuimarika kwa biashara ya kikanda chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Akiendelea na uchambuzi, Kibwana amesema katika muktadha wa diplomasia ya uchumi, uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Rwanda umeimarika kwa kiasi kikubwa, ambapo takribani asilimia 70 ya mizigo inayoelekea Rwanda hupitia Bandari ya Dar es Salaam, jambo linaloifanya Tanzania kuwa mhimili mkuu wa uchumi wa Rwanda.
Ameongeza kuwa “Tanzania na Rwanda zinaweza kusemwa kuwa na maslahi ya kibiashara yaliyofungamana,” hali inayochochea haja ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi na kuongeza ufanisi wa mifumo ya forodha na usafirishaji.
Katika upande wa miundombinu, makubaliano ya kuendeleza mradi wa reli ya kisasa ya SGR kuelekea Kigali yanatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati itakayobadilisha kabisa sura ya biashara ya ukanda huu kwa kupunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mizigo.
Katika uwanja wa diplomasia na usalama wa kikanda, ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda umeendelea kuimarisha utulivu wa mipaka na uratibu wa masuala ya kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, hali inayosaidia mazingira salama ya biashara na uwekezaji.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda umejengwa katika msingi wa undugu na ujirani mwema, ambapo biashara kati ya nchi hizo imefikia thamani ya shilingi bilioni 644 mwaka 2025.
Amebainisha pia kuwa kuanzia mwaka 1990 hadi Machi 2026, Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5, iliyozalisha zaidi ya ajira 2,225 kwa Watanzania, hali inayoonesha matokeo halisi ya Diplomasia ya Uchumi.
Katika sekta ya nishati, Rais Samia amesema miradi ya kikanda kama Maporomoko ya Umeme ya Rusumo pamoja na ushirikiano kati ya TANESCO na Rwanda Energy Group inaendelea kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa ajili ya viwanda na maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Rais Paul Kagame amesisitiza kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa kimkakati, hasa katika sekta ya uchukuzi na biashara kupitia Bandari ya Dar es Salaam, akieleza kuwa uhusiano huo ni msingi muhimu wa maendeleo ya nchi zote mbili.
Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kuimarisha zaidi ushirikiano katika miradi ya kimkakati ikiwemo SGR, nishati na uwekezaji wa viwanda, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa kikanda kupitia EAC, Umoja wa Afrika na majukwaa ya kimataifa.
Kwa ujumla, ziara ya Rais Kagame nchini Tanzania imeelezwa na wachambuzi kuwa imeongeza nguvu katika Diplomasia ya Uchumi, kuimarisha ushirikiano wa biashara, miundombinu na nishati, na kuweka msingi imara wa Tanzania kuendelea kujikita kama kitovu cha biashara na diplomasia ya kikanda Afrika Mashariki.
