Na Jackline Minja, WMMJW Mtwara

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesisitiza umuhimu wa malezi na makuzi bora kwa watoto, akieleza kuwa ndiyo msingi wa kujenga kizazi chenye maadili, afya njema, elimu na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na Taifa.

Akizungumza katika nyakati tofauti tarehe 1Julai, 2026 mkoani Mtwara, Naibu Waziri Mahundi amesema malezi ya mtoto ni jukumu la wazazi wote wawili, hivyo akawataka akina baba na akina mama kushirikiana kwa karibu katika kuwalea watoto wao badala ya kumwachia mzazi mmoja jukumu hilo.

“Malezi ya mtoto si jukumu la mama pekee, Baba na mama wanapaswa kushirikiana kwa upendo, uwajibikaji na mshikamano ili kuwajengea watoto msingi imara wa maisha kwa kuwa watoto wa leo ndiyo viongozi na nguvu kazi ya kesho, hivyo wanahitaji kulelewa katika mazingira salama na yenye maadili mema,” amesema Naibu Waziri Mahundi.

Aidha, Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi yanayowainua wananchi kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za uwezeshaji, hivyo amewahimiza wajasiriamali kutumia kikamilifu mikopo inayotolewa kupitia mabenki na taasisi za kifedha ili kukuza biashara zao, kuongeza kipato na kuboresha ustawi wa familia.

“Mikopo inayotolewa na Serikali ni fursa ya kujiletea maendeleo nawahimiza wajasiriamali kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili biashara zikue, kipato kiongezeke na hatimaye familia ziwe na uwezo wa kuwapatia watoto huduma bora za elimu, afya na lishe.” amesema Naibu Waziri Mahundi.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mahundi amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, kwa kuanzisha kituo cha kulelea watoto katika Soko la Chuno, akieleza kuwa kituo hicho ni mfano wa ubunifu unaowasaidia wazazi, hususan wajasiriamali, kutekeleza shughuli zao za kiuchumi huku watoto wao wakipata huduma ya uangalizi katika mazingira salama.

Naibu Waziri Mahundi amesema uwepo wa kituo hicho umeleta nafuu kwa wazazi wanaofanya shughuli za biashara sokoni hapo, huku ukiwa sehemu ya jitihada za kuhakikisha watoto wanapata malezi na ulinzi stahiki wakati wazazi wao wakitafuta kipato cha kuendesha maisha ya familia.Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Joel Nanauka, amesema elimu hiyo itaongeza uelewa wa jamii na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kujenga familia imara na Taifa lenye maendeleo endelevu.