MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akizungumza kwenye hafla hiyo jijini Arusha.
……..
Na Happy Lazaro, Arusha 
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amekabithi vitanda 80 na magodoro 160 kuboresha huduma za Sober houses Arusha  katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Aidha msaada huo umetolewa na DCEA   kwa kushirikiana na  NSSF, PSSSF   ambapo lengo ni kurejesha matumaini kwa waathirika, kulinda nguvu kazi ya taifa na kujenga jamii yenye afya.
Akizungumza wakati wa kukabithi misaada huo ,Mkude amewataka vijana nchini kujiepusha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya akisisitiza kuwa dawa hizo si njia ya mafanikio bali ni chanzo cha kuharibu ndoto, afya na mustakabali wa maisha ya vijana wengi.
Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43 umetolewa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa ufadhili wa mifuko ya hifadhi ya iamii ya NSSF na PSSSF, ikiwa ni sehemu ya arisha huduma kwa waraibu wanaopata tiba na uangalizi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkude alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia huduma za tiba, kinga na uangalizi ikiwemo vituo vya MAT, Sober Houses na huduma za afya ya akili.
Amesema lengo ni kurejesha matumaini kwa waathirika, kulinda nguvu kazi ya taifa na kujenga jamii yenye afya.
“Matumizi ya dawa za kulevya si ujanja wala mafanikio, bali ni mwanzo wa kuangamiza ndoto, kuharibu afya na kupoteza mwelekeo wa maisha. Tunapaswa kushirikiana kupinga biashara na matumizi ya dawa hizi,” alisema Mkude.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Arusha una jumla ya nyumba 19 za upataji nafuu katika wilaya za Arusha Jiji, Arumeru, Karatu, Monduli na Longido zinazohudumia waraibu 505, wakiwemo wanawake 98 na wanaume 407.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Elimu wa DCEA, Sarah Ndaba, alisema mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia mikakati ya kupunguza upatikanaji, mahitaji na madhara ya dawa hizo.
Alisisitiza kuwa waraibu hawapaswi kunyanyapaliwa bali kusaidiwa kurejea katika maisha ya kawaida.
“Uraibu ni ugonjwa unaotibika. Jamii ina wajibu wa kuwapa nafasi ya pili waraibu badala ya kuwanyanyapaa,” alisema Ndaba.
Alibainisha kuwa ukaguzi wa DCEA ulibaini uhaba wa vitanda na magodoro katika baadhi ya vituo, hali iliyosababisha wadau kuhamasishwa kusaidia, ambapo NSSF na PSSSF walijitokeza kwa haraka.
KAIMU Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Abubakar Soud, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali na wadau katika kusaidia makundi maalum yakiwemo waraibu wa dawa za kulevya.
“Tunajenga maisha ya sasa na baadaye. Huu ni uwekezaji katika utu na ustawi wa jamii,” alisema Soud.
Alibainisha kuwa NSSF imechangia manunuzi ya vitanda 80 na magodoro 160 na itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kusaidia miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa na misaada mbalimbali.
Katika tukio hilo, mrahibu wa dawa za kulevya, Maita Chacha, alitoa ushuhuda wa maisha yake ya uraibu wa takribani miaka 15, akieleza jinsi alivyopoteza elimu, ajira na mwelekeo wa maisha.
“Niliishi maisha ya kutangatanga na nilifikia hatua ya kukata tamaa. Lakini baada ya kupata huduma za Sober House nilianza kurejea katika maisha ya kawaida,” alisema Chacha.
Alisema mfumo wa waraibu waliopona kusaidia wenzao umeonyesha mafanikio makubwa na kuwataka wanaopata nafuu kuendelea kusaidiwa ili kuepuka kurudia matumizi ya dawa hizo.
Serikali pamoja na wadau wamesisitiza kuendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya huku wakihimiza jamii kuwasaidia waraibu badala ya kuwanyanyapaa, wakibainisha kuwa urejeshaji wa utu na afya ya jamii ni jukumu la pamoja.