Na Atley Kuni, WAF-Mwanza

Waziri wa Afya, Mhe.Mohamed Mchengerwa, ametoa maelekezo mahsusi kwa wananchi na wadau wa sekta ya afya kuamka na kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza bila aibu ili kuilinda jamii ya kitanzania. 

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Mei 4, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya “Jua Namba Zako”, akisisitiza kuwa wananchi wakitambua namba zao mapema wataweza kuwa walinzi wa kwanza wa afya zao. 

“Kampeni hii ni hatua muhimu na ya kimkakati katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, lengo kuu ni kuzuia na kugundua magonjwa mapema kabla hayajaleta madhara makubwa kwa wananchi”, amesema Mhe. Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa serikali inalenga kujenga mfumo wa afya unaomtangulia mgonjwa badala ya kusubiri ugonjwa ukue, hatua itakayosaidia kujenga kesho bora kwa wananchi wenye afya njema.

Katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma, Waziri huyo amesema kuwa kampeni hiyo imezingatia makundi yote ya kijamii bila ubaguzi, ikiwemo jinsia, umri, eneo analoishi mtu pamoja na kiwango cha elimu na rangi.

Aidha, amewataka wananchi kuchukua hatua madhubuti kwa kufanya upimaji wa afya mara kwa mara, akisisitiza umuhimu wa kufuatilia shinikizo la damu, kiwango cha sukari, uzito wa mwili ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wa wataalamu wa afya, Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, pamoja na wataalamu wengine kushirikiana na vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu ya kina kwa jamii. 

Akizungumzia ugonjwa wa homa ya ini, Waziri huyo amesema jitihada za kutafuta rasilimali kupitia wadau wa maendeleo ili kupanua huduma za upimaji, matibabu na chanjo kwa wananchi, huku akinukuu kauli ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kuwa mipango ya maendeleo huhitaji ushirikiano wa wadau ili kufanikisha utekelezaji wake kwa haraka.

Amesisitiza kuwa, wananchi hawapaswi kuwa wapokeaji wa huduma tu bali washiriki hai, kwa kuuliza, kuelewa na kujua hali zao za afya wanapofika katika vituo vya kutolea huduma. 

Kupitia Kampeni ya *“Jua Namba Zako”*, Serikali inalenga kuwezesha wananchi kuelewa hali zao za afya na kuchukua hatua mapema, ili kudhibiti na kupunguza madhara ya magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini