Na.Sophia Kingimali.
Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wametajwa kuwa kiungo muhimu kinachoweza kuziba pengo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira, hatua itakayosaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza katika hafla ya Alumni Breakfast iliyofanyika leo Mei 4,2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, amesema ushiriki wa alumni unaweza kuwa chachu ya mafanikio kwa wanafunzi kwa kuwapatia uzoefu wa vitendo, mafunzo na hata fursa za ajira.
Amesema kupitia mitandao ya wahitimu, wanafunzi wanaweza kupata mwongozo sahihi wa taaluma na mahitaji ya soko, jambo linalosaidia kuwaandaa vizuri zaidi wanapohitimu masomo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Mwalimu Nyerere Kibaha, Profesa Marcellina Chijoriga, amesema alumni wana nafasi ya kipekee ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa kutumia taaluma na uzoefu wao.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, huku akiwataja wahitimu kama rasilimali muhimu inayoweza kusaidia kuboresha sekta ya elimu na uchumi kwa ujumla.
“Alumni wanaweza kusaidia kwa kutoa mafunzo kwa vitendo, ajira, ushauri wa kitaaluma na hata kushiriki katika tafiti na ubunifu,” amesema Prof. Chijoriga.
Aidha, amewahimiza wahitimu kuzingatia ujasiriamali badala ya kutegemea ajira rasmi pekee, akieleza kuwa kuanzisha biashara kutachochea ukuaji wa uchumi na kupunguza tatizo la ajira.
Prof. Lwoga ameongeza kuwa ushiriki wa alumni katika shughuli za maendeleo ya chuo, ikiwemo ufadhili wa masomo na ushauri wa kimkakati, unasaidia kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
Katika hafla hiyo, wahitimu walipata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano wao, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza umoja wao kwa manufaa ya wanafunzi na taasisi.
Baadhi ya wahitimu, akiwemo Ally Mayai Tembele na Jackline Michael, wamesema mikutano yao ya kila mwaka inalenga kuimarisha mtandao wao na kutumia uzoefu walionao kusaidia kizazi kipya cha wanafunzi kufikia malengo yao.

