Kutoka Pemba, Unguja, Mji mkongwe, Bagamoyo, Kondoa, Magofu ya kilwa, paa la mlima kilimanjaro na maeneo mengine ya Tanzania, wadau wa urithi wa dunia wamekutana katika Makumbusho ya Urithi Geopark Karatu Mkoani Arusha yanayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuadhimisha Urithi wa Dunia Afrika yaliyoanza leo tarehe 04/05/2026 hadi tarehe 05/05/2026.
Wakiwa katika jengo la makumbusho ya Urithi Geopark Wadau hao wameelezwa jinsi Ngorongoro ilivyo ni utajiri wa urithi wa dunia kutokana na uumbwaji wake uliotokana na mlipuko wa volcano zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita na kutengeneza kasoko iliyokusanya asili, uhai wa binadamu, mifumo ya ikolojia, na ustawi wa viumbe mbalimbali.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru amewashukuru wadau wote hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuipa fursa Ngorongoro kuandaa na kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu.
Wadau wa urithi wa duania wakiwa katika Makumbusho ya Urithi Geopark walipata fursa ya kuelezewa kuhusu uthibitisho wa wasomi unaoeleza wazi historia ya chimbuko la binadamu wa kale aliyepatikana katika bonde la olduvai takribani milioni 2 iliyopita na ushahidi wa Nyanyo za binadamu wa kale katika eneo la Laetoli takribani miaka 3.6 iliyopiTa ambapo binadamu hao walitembea kwa miguu miwili.
Taasisi zinazoshiriki maadhimisho hayo ambazo zinasimamia maeneo ya urithi wa dunia ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Mamlaka ya Uzimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma za misitu Tanzania (TFS), pamoja na wawakilishi wa maeneo ya urithi wa dunia kutoka Zanzibar.

