Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa ufadhili wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.277 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa vipande vya Makutupora–Tabora na Tabora–Isaka vyenye jumla ya kilometa 533.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo , Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar amesema kuwa ufadhili huo umetolewa kupitia mpango wa pamoja kutoka nchi za Italy, Sweden na Poland kupitia taasisi zao za dhamana za mikopo ya mauzo ya nje kwa uratibu wa Benki ya Standard Chartered.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika Aprili 28, 2026 Jijini Dodoma, huku mgeni rasmi Katika hafla hio akiwa ni Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar.
Aidha, Mkataba huo ni baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wabia wa maendeleo kutoka Italy, Sweden pamoja na Poland kupitia taasisi za SACE, EKN na KUKE chini ya uratibu wa Standard Chartered.
Amesema kuwa uwekezaji huo unaendeleza moja ya miradi ya kimkakati katika historia ya Tanzania uliolenga kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kanda ya Ziwa pamoja na nchi jirani huku ukiimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Aidha, amebainisha kuwa mradi huo siyo tu uwekezaji mkubwa wa miundombinu bali ni sehemu ya dira ya muda mrefu ya maendeleo ya Taifa kwa kuchochea ukuaji wa uchumi, biashara na usafirishaji.
Pia ameongeza kuwa matumizi ya reli hiyo kwa nishati ya umeme yataisaidia Tanzania kupunguza matumizi ya mafuta pamoja na uzalishaji wa hewa ukaa na hivyo kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua kubwa ya kihistoria itakayoiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha kisasa cha usafirishaji na usambazaji wa mizigo kikanda.
Amesema kuwa tangu kuanza kwa mradi wa SGR mwaka 2017 zaidi ya kilometa 2,100 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi huku kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma tayari kikianza kutoa huduma.
Aidha, amebainisha kuwa huduma ya treni kati ya Dar es Salaam na Dodoma tayari imesafirisha mamilioni ya abiria pamoja na tani za mizigo huku ikipunguza muda wa safari kutoka saa 12 hadi saa 3 pekee.
Pia ameongeza kuwa mradi huo utaongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafiri, kufungua fursa mpya za biashara na kuunganisha mikoa ya kati pamoja na Kanda ya Ziwa na nchi jirani.





