MHESHIMIWA Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameihakikishia Jamhuri ya Belarus kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na nchini hiyo na kwamba amewaalika wawekezaji na wafanyabiashara kuja nchini kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta za kilimo, uvuvi, elimu na afya.
Kauli hiyo imetolewa leo (Jumanne, Aprili 28, 2026) na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Pia, Dkt. Mwigulu amepokea kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaliko wa ziara ya kikazi nchini Belarus wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Belarus, Mheshimiwa Alexander Lukashenko.
Waziri Mkuu, amesema Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, pia Tanzania kibiashara ipo katika eneo la kimkakati kijiografia kwa kuwa ni kitovu cha Mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki na ya Kusini mwa Afrika.
“Ni kutokana na umuhimu huo, Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imejiwekea lengo la kuwa tegemeo la kanda hizo katika sekta ya kilimo sanjari na sekta ya afya ambayo Dira 2050 inataka Tanzania ijitosheleze katika uzalishaji wa dawa kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2050.” Amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Belarus katika sekta hizo utakuwa na matokeo chanya na ya haraka kutokana na nchi ya Belarus kupiga hatua katika sekta hizo, hasa matumizi ya teknolojia kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya dawa na zana za kilimo.
“Tutaangalia uwezekano wa kubadilishana wataalam kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo, ambapo Tanzania itatuma wataalam wa kilimo nchini Belarus ili wapate ujuzi, mfano katika teknolojia ya uundaji matrekta ya kisasa na zana nyingine za kilimo.” Ameongeza Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov ameeleza kuwa Serikali ya Belarus ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, elimu, sayansi na teknolojia.
“Nimefanya mazungumzo na mawaziri wa sekta muhimu hapa Tanzania, wakiwemo Waziri wa Elimu, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ambapo kwenye eneo la uvuvi tumeona fursa ya kuwa wananuzi wazuri wa mazao ya baharini kwani Tanzania yanapatikana kwa wingi.”
Ameongeza kuwa Belarus na Tanzania zinatarajiwa kusaini mikataba ya makubaliano (MoU) kuhusu kuwa na Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Belarus.“Makubaliano hayo yatawawezesha wafanyabiashara wa Tanzania na wa Belarus kuendesha shughuli zao kirahisi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.”
Wakati akikabidhi ujumbe wa mwaliko wa ziara ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Belarus, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov amesema pia Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania hivi karibuni.





