Na Mwandishi wetu, Kiteto
MKUU wa Wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Remidius Mwema amewapongeza jitihada zilizopelekea kubaini uwepo wa mashamba ya Bangi Wilayani humo huku amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kukabiliana na ulimaji wa bang huku akipongeza jitihada za utoaji taarifa zinazosaidia kubaini uwepo wa mashamba hayo.
Mhe.Mwema ameyasema hayo katika operesheni maalum ya kuteketeza dawa za kulevya aina ya bangi kufuatia uwepo wa mashamba yenye ukubwa wa takribani ekari tano (5) katika kitongoji cha Kimaraunga, Kijiji cha Mbigiri kata ya Partimbo Wilayani Kiteto.
Akiambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, na kushirikiana na viongozi wa vijiji na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, Mhe.Mwema amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha linawakamata watuhumiwa wote ikiwa ni pamoja na wamiliki wa mashamba hayo huku akisisitiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili sheria ichukue mkondo wake.
“Tumeshirikisha wananchi katika zoezi la kuteketeza dawa za kulevya ili kuonyesha kwa vitendo dhamira njema ya Serikali katika mapambano haya na tunatuma ujumbe kwa wananchi wote kuendelea kukabiliana na hali hii, operesheni hizi zitaendelea wakati wote ndani ya Wilaya yetu ,wananchi waendelee kutoa ushirikiano,” amesema Mhe. Mwema.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwema amesema
Serikali imewekeza nguvu kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na jamii kwa ujumla hatua ambayo imeendelea kuleta mafanikio makubwa katika kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa hizo hatarishi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapohisi au kushuhudia viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya kwa vyombo husika ili kuifanya Wilaya ya Kiteto na nchi ya Tanzania kuwa mahali salama dhidi ya matumizi na biashara ya dawa hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbigiri Omari Athumani Goda ameeleza utayari wao kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya huku akitoa ahadi ya kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha wamiliki wa mashamba hayo wanapatikana mara moja ili taratibu za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mbigiri, wamepongeza jitihada za Serikali katika kuteketeza kwa moto dawa hizo za kulevya na kuepuka athari katika jamii ikiwemo kupoteza nguvu kazi ya Taifa hususani kundi kubwa la Vijana.




