Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai, amesema kuwa ushirikiano kati ya taasisi hiyo na wanahabari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wa dawa na huduma za afya nchini.
Amesema hayo wakati wa ufunguzi wa semina kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na waandishi wa habari , akisisitiza kuwa sekta ya afya inahitaji uwazi na mawasiliano madhubuti ili kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi.
Tukai ameeleza kuwa MSD ina jukumu la kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa gharama nafuu ili kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameongeza kuwa mafanikio ya sekta ya afya yanategemea pia namna ambavyo vyombo vya habari vinavyowasilisha taarifa kwa umma, hivyo kuwataka wanahabari kutumia taaluma yao kwa weledi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao kazi hicho kati ya Wahariri na MSD Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Mgaya Kingoba, amesema wanahabari wanapaswa kufuata misingi ya taaluma kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya uandishi wa habari.
Kingoba ameeleza kuwa Bodi hiyo imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kwa lengo la kusimamia taaluma hiyo na kuhakikisha inazingatia viwango vinavyotakiwa.
Amesisitiza kuwa uwepo wa taratibu na miongozo si kwa ajili ya kuzuia uhuru wa vyombo vya habari, bali ni kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma.
Hivyo akawataka wahariri hao kuhakikisha wanapeleka habari zilizofanyiwanuchambuzi wa kutosha na zenye viwango ili kupeleka uelewa wa kutosha kwa wananchi badala ya kupeleka taharuki
Aidha, amewahakikishia wanahabari kuwa wanapaswa kujisikia huru kushiriki kikamilifu katika mijadala na kuuliza maswali yatakayosaidia kuboresha uelewa wa sekta ya afya.
Kwa upande Immaculate Makilika mwakilishi kutoka Idara ya Habari – Maelezo amesema serikali itaendelea kushirikiana na wanahabari ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na zenye uwiano.
Amehitimisha kwa kuipongeza MSD kwa kuandaa semina hiyo, akisema ni jukwaa muhimu la kujenga uelewa wa pamoja kati ya Bohari ya Dawa MSD na wadau wa habari katika kuimarisha sekta ya afya nchini
Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya, Mfamasia Mwandamizi Aneth Wilbroad , amesema wanahabari ni daraja muhimu kati ya serikali na wananchi katika kufikisha taarifa za afya kwa usahihi.
Amesema kupitia semina hiyo, wanahabari watapata uelewa mpana kuhusu shughuli za MSD na juhudi za serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Waziri Mkuu Tamisemi, Bw. Idrissa Hassan ambaye ni Afisa Maabara amesema taasisi hiyo ina jukumu la kutafsiri sera za wizara za kisekta na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Ameongeza kuwa Tamisemi pia inasimamia utekelezaji huo pamoja na kukusanya maoni na changamoto kutoka kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.





