Na Mwandishi Wetu, Kakonko
Mnamo Aprili 21, 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Kakonko, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mhe. A. J. Kyamba (SRM), shauri la uhujumu uchumi namba ECC 8474/2026 limefunguliwa, likiwahusu Abubakari Salumu Choyo (32), mwalimu wa Shule ya Msingi Kiyobera, na Mohamedi Miraji Ramadhani (35), aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo.
Shauri hilo, linaloendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Bw. Abdulrahim Omari, linawahusisha washtakiwa na makosa ya rushwa pamoja na kughushi nyaraka kinyume na sheria mbalimbali za nchi, ikiwemo Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA) na Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Inadaiwa kuwa Januari 11, 2025, Abubakari Salumu Choyo aliandaa dokezo la kuomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 334,000 kwa madai ya kulipa wapishi, mwalimu wa kujitolea na gharama za sukari, huku akijua kuwa watu waliotajwa hawakuwepo shuleni hapo.
Aidha, upande wa mashtaka umeeleza kuwa Mohamedi Miraji Ramadhani aliandaa nyaraka za uongo, ikiwemo mkataba wa kazi, kuonesha kuwa malipo ya shilingi 160,000 yalifanyika kwa watu ambao hawakuwa wakifanya kazi husika. Pia alipitisha dokezo hilo licha ya madai hayo kuwa si ya kweli.
Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa wa kwanza alikiri kosa la kwanza, huku mshtakiwa wa pili akikana makosa yote.
Washtakiwa wote wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Aprili 27, 2026, litakaposikilizwa tena kwa ajili ya hatua za awali (PH).




