Na Mwandishi Maalum,
Tunduru
WAKULIMA wilayani Tunduru,wamekipongeza chama kikuu cha ushirika(TAMCU)kwa kununua magari makubwa mapya matano ya kubebea mizigo ambayo yatasaidia kupunguza adha ya kuchelewesha mazao yao kwenda mnadani na kushindwa kupata fedha kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake Rashid Chibwana alisema,magari hayo yatarahisisha na kutumikia wakulima kwa kuwafikia walipo kwa ajili ya kusafirisha mazao kutoka mashambani na kupeleka kwenye maghala kabla ya kuuzwa kwenye minada.
“Tunawashuru sana viongozi wa chama chetu Tamcu kwa kuongeza miradi ya chama chetu,huko nyuma tulitegemea chanzo kimoja tu cha mapato ambacho ni ushuru,lakini magari haya yatakuwa chanzo kikubwa cha mapato na kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayolimwa na kukusanywa na vyama vyetu kutoka kwa wakulima”alisema Chibwana.
Alisema, katika wilaya ya Tunduru kuna uhaba mkubwa wa magari ya kubebea mazao na yaliyopo ni mabovu hivyo yanashindwa kufikisha mazao kwenda kwenye maghala ya chama kikuu kwa wakati.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika(Tamcu)Mussa Manjaule alisema,ununuzi wa magari hayo ni utekelezaji wa maagizo ya wanachama ambao waliitaka bodi ya chama hicho kununua magari ya mizigo ili yasaidia kubeba mazao na kuwa chanzo cha mapato.
Manjaule alisema,awali walikuwa wanapata shida kuleta viuatilifu kutoka mkoa jirani wa Mtwara kuleta Tunduru kwa ajili ya wakulima,lakini kwa sasa magari hayo yatakuwa mkombozi kwa wanachama na wakulima wengine wa wilayani Tunduru.
Kwa upande wake meneja wa CRDB Tawi la Tunduru Emanuel Mwasuka alisema,gharama ya magari hayo ni Sh.bilioni 1.5 kati ya hizo CRDB imetoa kiasi cha Sh.735 na Chama kikuu kimechangia Sh.milioni 315.
Alisema,CRDB itaendelea kutoa mikopo ya fedha kwa vyama vikuu na vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)vyenye mahitaji kwani uchumi wa wilaya ya Tunduru unaendelea kukua kwa kasi kubwa,hivyo mahitaji ya magari kwa ajili ya kubeba mazao ni bidhaa mbalimbali ni makubwa.
Amewataka viongozi wa Tamcu kuhakikisha wanatunza magari hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuongeza mapato ya chama ili kuleta tija kwa chama na wanachama.
“Faida kubwa ya magari haya ni chanzo kikubwa cha mapato kwa chama kikuu,hii ni fursa kubwa na mfano mzuri kwa vyama vingine vikuu katika mkoa wetu wa Ruvuma na mikoa jirani,ninavyokitazama chama kikuu Tamcu kitafika mbali zaidi na benki ya CRDB itaendelea kutoa mikopo kama kuunga mkono jitihada zao”alisema Mwasuka.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja,amekipongeza Chama kikuu kwa kutekeleza maadhimio ya kununua malori hayo ambayo yatapunguza kero ya kusafirisha mazao ya wakulima kutoka mashambani na kupeleka kwenye maghala ya vyama vya msingi vya ushirika.
Alisema,ununuzi wa malori hayo ni hatua kubwa katika sekta ya usafirishaji,kuongeza ufanisi wa biashara ya korosho,ufuta na mbaazi mazao yanayolimwa kwa wingi na kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza tija kwa wanachama.
“Haya ni maendeleo na mfano bora katika sekta ya ushirika unaoweka mbele maslahi ya wanachama,nawaomba wanachama muwape ushirikiano viongozi wa Tamcu hususani mwenyekiti,wajumbe wa bodi na watumishi ili waendeleaa kufanya mambo makubwa zaidi kwa manufaa yenu wanachama na wakulima”alisema Masanja.
MWISHO.
Picha no 745 Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja katikati,akikata utepe kuzindua malori matano mapya ya Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu)ambayo ni mkopo kutoka Benki ya Crdb,kushoto meneja wa Crdb Tawi la Tunduru Emanuel Mwasuka,wa pili kushoto meneja biashara wa Benki hiyo kanda ya kusini Emanuel Biganio na wa tatu kulia Mwenyekiti wa Tamcu Musa Manjaule.
Picha no 748 Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja kushoto,akikabidhi mfano wa funguo za magari matano mapya aina ya Howo kwa Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani humo Marcelino Mrope kwa ajili yaliyonunuliwa na chama hicho ili kubeba mazao ya wanachama na wanachi wengine,katikati Mwenyekiti wa Tamcu Musa Manjaule.
Picha no753Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru (Tamcu) Musa Manjaule kushoto na meneja masoko wa Benki ya Crdb kanda ya kusini Emanuel Bigailo wakisaini hati ya makabidhiano ya malori matano mapya yaliyonunuliwa na Tamcu baada ya kupata mkopo kutoka Crdb,nayeshuhudia katikati Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Deni Masanja.





