Kigoma, Aprili 17, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe.Balozi Simon Sirro, ametoa wito kwa wateja na wadau wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tabora kuhakikisha wanasimamia ipasavyo mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwezesha ulipaji wa madeni kwa wakati na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha wateja na wadau wa MSD Kanda ya Tabora kilichofanyika mkoani Kigoma, Balozi Sirro alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa kifedha katika sekta ya afya, akieleza kuwa usimamizi dhaifu wa mapato unachangia ucheleweshaji wa malipo na hivyo kuathiri mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.
“Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha mapato yanakusanywa na kutumika ipasavyo ili taasisi kama MSD iweze kuendelea kutoa huduma bora bila vikwazo vya kifedha,” alisisitiza Sirro.
Pia, aliwahimiza wadau hao kushiriki majadiliano yenye tija na MSD ili kila upande uweze kutekeleza wajibu wake kikamilifu. Aliongeza kuwa ni muhimu kufanya maoteo sahihi, pamoja na kutoa mrejesho wa huduma ili kubaini na kutatua changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD, Bw.Hassan Ally, aliwahakikishia wadau hao kuwa taasisi hiyo inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuboresha huduma zake. Alieleza kuwa MSD inalenga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wakati na kwa ubora kwenye zaidi ya vituo 9,000 vya kutolea huduma za afya nchini.
Alisisitiza kuwa hivi sasa MSD imeweza kufikisha bidhaa vituoni kwa wakati kwa asilimia 94, huku mahitaji ya wateja yakitimizwa kwa asilimia 83
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Tabora, Rashid Omary, aliwashukuru wateja na wadau wote waliohudhuria kikao hicho, akisisitiza kuwa majadiliano hayo ni muhimu katika kuimarisha huduma katika kanda hiyo inayohudumia mkoa wa Kigoma, Tabora na Katavi.
Alibainisha kuwa kanda hiyo inahudumia jumla ya vituo 884 vya afya, hivyo ushirikiano wa karibu kati ya MSD na wadau ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.





