Na.Sophia Kingimali.Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuongeza fursa za elimu nchini.
Pia,ametoa rai kwa wanufaika wote wa mikopo kuacha kusubiri kuwa na fedha nyingi ndipo waanze kulipa huku akisisitiza kuwa nidhamu ya kifedha ni muhimu kwa maendeleo binafsi na taifa.
Hayo ameyasema leo Aprili 17,2026 wakati wa akizindua kampeni ya Kiduchu,inayoendeshwa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HESLB)Wanu amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Amesema katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, serikali imetoa zaidi ya shilingi trilioni 3.6 kusaidia wanafunzi kusoma katika vyuo mbalimbali vya elimu ya kati na ya juu.
Aidha Wanu ameeleza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea kwa kiasi kikubwa urejeshwaji wa mikopo ili kutoa nafasi kwa vizazi vijavyo kunufaika na mfuko huo.
Ameongeza kuwa hadi sasa, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imefanikiwa kukusanya takribani shilingi trilioni 1.4 kutoka kwa wanufaika katika kipindi cha miaka mitano.
Ameir amesisitiza kuwa kampeni ya Kiduchu inalenga kuhamasisha utamaduni wa ulipaji wa hiari, hata kwa kiasi kidogo, ili kupunguza mzigo wa madeni kwa wanufaika.
“Kiduchu ni kidogo kidogo; hata kiasi kidogo kinaweza kusaidia kurejesha mkopo na kutoa nafasi kwa wengine,” amesema Wanu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo(HESLB), Dk. Bill Kiwia, amesema jumla ya shilingi trilioni tisa zimetolewa kama mikopo kwa wanafunzi, huku sehemu kubwa ikiwa bado haijarejeshwa.
Amesema mikopo yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 2.7 tayari imeiva na inapaswa kurejeshwa na wanufaika zaidi ya laki tisa.
Dk. Kiwia ameongeza kuwa kampeni ya Kiduchu inalenga kuwafikia wanufaika wengi zaidi, hususan wale walioko katika sekta isiyo rasmi, ili kuongeza makusanyo na kuboresha uendelevu wa mfuko.
Amebainisha kuwa kampeni hiyo pia inalenga kujenga historia nzuri ya mikopo kwa wanufaika, jambo litakalowasaidia kupata huduma za kifedha katika taasisi mbalimbali.





