*Ni katika Kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa umeme
*Waishukuru TANESCO kwa zawadi hiyo, wapongeza kazi kubwa inayofanywa na Shirika
*Waahidi kwenda kuwa mabalozi wazuri wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Umeme
Na. Mwandishi Wetu, Manyara
Katika Kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa umeme hapa nchini Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange ametoa Majiko zaidi ya 30 kwa Walimu wa Shule ya Wasichana Mkoa wa Manyara ili kuwapa hamasa kwa kazi wanayoifanya.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhe. Fakii Lulandala amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange kwa kutoa majiko hayo kwa walimu yanayolenga kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa umeme.
Amesema Bw. Twange anaunga mkono kwa vitendo ajenda ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na TANESCO katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amesema majiko hayo yanakwenda kutoa motisha kubwa kwa walimu wa shule hiyo na kuchochea ari ya ufundishaji kwa wanafunzi kwani sasa watatumia muda mchache wakati wa kupika hali ambayo itasaidia kuongeza ufaulu zaidi kwa wanafunzi hao.
Amesema licha ya kutoa Majiko hayo Bw. Lazaro Twange anamchango Mkubwa katika ujenzi wa Shule hiyo ya Wasichana kwani alihakikisha anaisimamia kikamilifu wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Babati na kufanikisha ujenzi wake kutokana na kujitoa kwakwe usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unakamilika.
“Bw. Lazaro Twange ndiye kinara wa ujenzi wa Shule hii na leo ametoa majiko ya kisasa yanayotumia umeme kidogo sana kwa ajili ya kuwagawia walimu, na hii inakwenda kuwa motisha kubwa kwa walimu wa shule hii hasa katika matumizi ya Nishati Safi ya umeme “
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Manyara Mhandisi Regina Mvungi amesema kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange wamekabidhi majiko 30 kwa walimu wa shule hiyo kama zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO.
Amesema majiko hayo yamekabidhiwa kwa walimu wote wa Shule hiyo na sasa wanakwenda kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa umeme kwa vitendo kwa jamii inayowazunguka wakiwemo wanafunzi wao na wananchi kwa ujumla.
“Kupitia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange tumetoa zawadi ya majiko 30 kwa walimu wa shule hii ili wakawe mabalozi wa kupikia kwa umeme kuanzia shuleni na jamii zinazowazunguka”
Naye Mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Mkoa wa Manyara Mwl. Gisela Msoffe amelishukuru Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Babati hasa kwa usimamizi uliotukuka wa ujenzi wa shule hiyo pamoja na kuwezesha kufikishiwa kwa huduma ya umeme katika majengo yote ya shule hiyo.
Zaidi ameshukuru kwa zawadi ya majiko ya kisasa ya umeme waliyopatiwa walimu kwani yanakwenda kuwa msaada mkubwa hasa katika kuokoa muda wakati wa kupika ili kuwawezesha kuwa na muda wa kutosha kufundisha wanafunzi.
“Nimshukuru kwa dhati Bw. Lazaro Twange watumishi wote wa shule hii hasa Walimu tumepewa majiko ya kisasa ya umeme yatatusaidia kuokoa muda wakati wa kupika na tutapata Muda mwingi wa kufundisha Wanafunzi” ameongeza Mwl. Gisela





