Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma

‎Katika mwendelezo wa kuimarisha usalama wa mabwawa ya maji na yale ya tope sumu (TSF) migodini, Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) na Kampuni ya City Engineering imeandaa mafunzo ya siku tatu yatakayoshirikisha wataalam kutoka kwa wamiliki wa migodi, wamiliki wa mabwawa makubwa ya maji, wataalam waliosajiliwa (Approved Professional Persons – APPs) na watendaji wa Serikali wanaohusika na usimamizi wa mabwawa.

‎Mafunzo hayo yatafanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2026. Mwaka huu, mafunzo yatajikita katika Usalama wa Miundombinu ya Mabwawa (Managing Critical Infrastructures for Dam Safety) kuanzia hatua ya usanifu, utumiaji hadi ufungaji.

‎hayo yameelezwa Machi 31,2026  na Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Bw. Robert Sunday, akimwakilisha Katibu Mkuu Wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, wakati akizungumza na waandishi wa Habari Katika Ukumbi wa Mikutano wa wizara ya Maji mji wa Mtumba.

‎Akizungumza kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo, Bw. Robert Sunday amesema mabwawa ya maji na tope sumu husanifiwa na ukomo wa uhai wake (life span). Hata hivyo, ili kuongeza uhai wa mabwawa hayo na kuhakikisha yanaendelea kuwa salama, hatua mbalimbali zinahitajika, ikiwemo kuongeza ujuzi na maarifa ya wataalam katika mzunguko mzima wa miundombinu ya mabwawa.

‎“Mafunzo haya ni muhimu kwa kuwa yanalenga kuongeza ujuzi na maarifa katika mzunguko mzima wa miundombinu ya mabwawa, kuanzia usanifu hadi ufungaji,” amesema Bw. Sunday 

‎Bw. Sunday amewahamasisha watunga sera, wamiliki wa mabwawa, wataalam wa sekta ya maji, taasisi na wadau binafsi kujisajili kwenye mafunzo haya kupitia tovuti: https://damsafetyconference.tz

‎Kwa mujibu wa Bw. Sunday, kwa miaka minne mfululizo, mafunzo na mikutano ya usalama wa mabwawa yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa kushirikisha wadau kutoka sekta binafsi na wataalam kutoka mataifa yaliyoendelea katika usalama wa mabwawa. Ushirikiano huu umesaidia kulinda mazingira na rasilimali za maji nchini.

‎Aidha, Bw. Sunday amebainisha kuwa imeanza taratibu za Tanzania kujiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Usalama wa Mabwawa Makubwa (International Commission on Large Dams – ICOLD), hatua itakayoongeza uwezo wa kitaasisi na kiufundi wa Tanzania katika uhandisi na usimamizi wa mabwawa kwa usalama endelevu.

‎Mafunzo ya mwaka jana, yaliyofanyika Novemba 2025, yalikusanya washiriki zaidi ya 200 na yalijikita kwenye tahadhari za dharura na majibu ya haraka kwa majanga yanayohusiana na mabwawa ya maji na tope sumu, na kufundisha mbinu zilizofanikiwa nchini Afrika Kusini, nchi iliyopiga hatua kubwa katika usalama wa mabwawa.Bw. Sunday amesisitiza kuwa elimu hii na mafunzo ya mara kwa mara ni msingi wa kuhakikisha mabwawa yote nchini yanaendelea kuwa salama, rasilimali za maji zinahifadhiwa, na hatari za majanga zinapunguzwa.

‎Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Bw. Benjamini Mchwampaka, ameeleza kuwa mikutano na mafunzo ya kila mwaka yamekuwa fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya maji na madini kuungana, kubadilishana ujuzi na kukabiliana na changamoto zinazohusiana na usalama wa mabwawa. Amesistiza  kuwa ushirikiano huu unasaidia kulinda maisha ya watu, mali zao, na mazingira, huku wakishirikiana na wataalamu wa ndani na wa kimataifa.

‎kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa City Engineering, Bw. Anael Macha, ameongeza kuwa mkutano huo ni nafasi ya moja kwa moja kwa wadau wa sekta ya madini na maji kujadili, kuwasilisha bidhaa na huduma zao, na kupata uungwaji mkono wa kiufundi na kifedha. 

‎Mafunzo haya yanakuja sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025–2050, ikizingatia uadilifu wa mazingira, usalama wa mabwawa, na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na tope sumu, na kuimarisha jitihada za Tanzania katika kuhakikisha mabwawa yote yanaendelea kuwa salama.