VIONGOZI wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma watakiwa kusimamia misingi ya maadili na mawasiliano ili kulinda imani ya wananchi katika huduma wanazopewa.

Rai hiyo imetolewa wakati wa mafunzo maalumu ya uongozi yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, yakilenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika kusimamia rasilimali na kuhudumia umma kwa uadilifu, huku wakionywa kuwa mmomonyoko wa maadili duniani sasa ni tishio linalohitaji udhibiti wa pamoja.

Akiwasilisha mada kuhusu maadili na umuhimu wa mawasiliano katika uongozi, Mhadhiri kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo), Ng’omange Merkiad alisisitiza kuwa kuwepo kwa taratibu na kanuni madhubuti za kimaadili ni jambo la lazima ili kuwepo na tabia inayofanana na inayotabirika wakati wa kuwahudumia wananchi. “Maadili sio masimulizi tu ya maneno, bali ni maelekezo ya vitendo yanayomwongoza kiongozi kujua nini cha kufanya na kwa wakati gani katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ya kiutawala” alisema Merkiad.

Akizungumzia dhamana ya uongozi, aliwakumbusha viongozi hao wa mitaa kuwa nafasi walizonazo ni matokeo ya imani kubwa ambayo serikali imewekeza kwao, hivyo wanapaswa kuilinda imani hiyo kwa wivu mkubwa kwa kuishi maisha ya uadilifu. “Imethibitika bila shaka yoyote kwamba uadilifu ni nyenzo kuu inayomwezesha kiongozi kuishi katika usafi wa kiutendaji, jambo ambalo ni msingi mkuu wa kujenga na kuimarisha imani ya wananchi kuelekea kwa viongozi wao wa ngazi za chini. Tusichoke kuwa waadilifu kwasababu tutaokoa kizazi kijacho” alisema Merkiad.

Nae, Katibu wa Vijana Platform Halamshauri ya Jiji la Dodoma, Jamal Mshumbusi aliyehudhuria mafunzo hayo alipongeza na kubainisha kuwa yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi, uwajibikaji, na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.

Usimamizi thabiti wa maadili na matumizi ya mawasiliano ya uwazi, viongozi hao sasa wanatarajiwa kuacha alama chanya na kuimarisha utawala bora, hatua itakayochochea maendeleo ya haraka na endelevu kuanzia ngazi ya mitaa hadi taifa kwa ujumla.