Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw. Crispin Chalamila, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi, 2026.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema imefanikiwa kuokoa Shilingi bilioni 14.5 kupitia operesheni za uchunguzi katika mwaka wa fedha 2024/25, huku ikibainisha mafanikio na changamoto katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam leo Machi 30, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila alisema utendaji kazi wa taasisi hiyo ulijikita katika misingi ya kuzuia rushwa, kuelimisha umma, kufanya uchunguzi pamoja na kuendesha mashtaka.
“Utendaji kazi wetu ulizingatia misingi ya uzuiaji rushwa, uelimishaji umma, uchunguzi pamoja na uendeshaji wa mashtaka, kwa kuzingatia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 na miongozo mingine ya kitaifa,” alisema Chalamila.
Alisema katika mwaka 2024/25, TAKUKURU iliweka kipaumbele katika maeneo matatu ambayo ni ukusanyaji wa mapato ya Serikali, udhibiti wa rushwa katika uchaguzi pamoja na kudhibiti rushwa katika utoaji wa huduma kwa umma hususan sekta za afya, maji, elimu, ardhi na ujenzi.
Akizungumzia juhudi za kuzuia rushwa, Chalamila alisema taasisi hiyo ilifanya tafiti mbili na uchambuzi wa mifumo 757, ikiwa ni ongezeko kutoka kazi 660 zilizofanyika mwaka uliotangulia.
“Lengo la kazi hizi lilikuwa ni kubaini mianya ya rushwa na kutoa mapendekezo ya namna ya kuidhibiti mapema kabla haijasababisha hasara kwa umma,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa uchambuzi huo ulihusisha maeneo mbalimbali ikiwemo mapato ya ndani katika halmashauri 40, matumizi ya mashine za POS, usimamizi wa mipaka pamoja na mifumo ya kodi ya zuio katika miradi ya maendeleo.
Kutokana na uchambuzi huo, vikao 671 vya wadau vilifanyika na kuwezesha kuibuliwa kwa mikakati 3,470 ya kudhibiti rushwa ambapo mikakati 2,994 sawa na asilimia 86 ilitekelezwa huku mingine ikiendelea kufanyiwa kazi.
“Matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo yameongeza mapato ya halmashauri kwa zaidi ya Shilingi bilioni 8.6, yakiongezeka kutoka bilioni 97.8 hadi kufikia bilioni 106.4 kwa mwaka,” alisema.
Katika eneo la kodi ya zuio, Chalamila alisema kulibainika mapungufu katika baadhi ya halmashauri ambapo kodi haikukatwa au kuwasilishwa ipasavyo, ikiwemo Shilingi milioni 982.7 katika Iringa na Shilingi milioni 13.1 katika Meatu.
“Hata hivyo, baada ya ufuatiliaji wetu, kiasi chote cha kodi ambacho hakikukatwa au kuwasilishwa, kilikusanywa na kupelekwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alieleza.
Aliongeza kuwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki yameleta tija ambapo Halmashauri ya Rombo iliongeza makusanyo kwa asilimia 100 kupitia mashine za POS, kutoka Shilingi bilioni 2.2 hadi kufikia bilioni 4.4.
Kuhusu ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, alisema TAKUKURU ilifuatilia miradi 1,864 yenye thamani ya Shilingi trilioni 14.3 ambapo miradi 913 ilibainika kuwa na kasoro na 66 ilianzishiwa uchunguzi.
“Bado kuna changamoto ya usimamizi dhaifu wa mikataba unaosababisha malipo ya kazi ambazo hazijatekelezwa, ubora hafifu wa miradi na ukiukwaji wa taratibu za ununuzi wa umma,” alionya.
Katika Programu ya TAKUKURU Rafiki, alisema jumla ya kero 25,061 ziliibuliwa ambapo 10,785 zimetatuliwa na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Akizungumzia uelimishaji umma, Chalamila alisema semina 4,760 na mikutano ya hadhara 4,143 ilifanyika huku klabu za wapinga rushwa zikifikia 7,042 zenye wanachama 996,807.
“Hii inaonesha mwitikio mkubwa wa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na kuendelea kujenga utamaduni wa kuichukia rushwa,” alisema.
Kwa upande wa uchunguzi, alisema majalada 1,030 yalikamilika mwaka 2024/25 yakiwemo 22 ya rushwa kubwa yenye thamani ya Shilingi bilioni 210.5.
Aidha, alibainisha kuwa uchunguzi maalum uligundua wizi wa Shilingi bilioni 147.5 kupitia kadi 1,551 za benki kutoka mataifa 11, huku watuhumiwa wakisababisha hasara ya Shilingi bilioni 2.6 kwa baadhi ya taasisi za fedha.

