Diwani wa Kata ya Makuburi, Mhe. Issa Faru (kulia) akikabidhi vyeti vya pongezi kwa viongozi  wa  Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kata ya Makuburi ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa baadhi ya viongozi watawi wa jumuiya hiyo kwa mwaka 2025.

Katibu wa UWT Kata ya Makuburi, Bi. Severina Minga (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa UWT Kata hiyo, Bi. Editha Ngotanile wakiongoza kikao cha Baraza la UWT  kilichofanyika 17 Januari, 2026 jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa Baraza la UWT Kata ya Makuburi wakiwa katika kikao.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la UWT Kata ya Makuburi wakiwa katika picha ya pamoja na Diwani wa Kata hiyo

……………………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kata ya Makuburi imefanya kikao cha Baraza la Kata, pamoja na kutoa vyeti vya pongezi kwa baadhi ya viongozi wa ngazi ya matawi waliofanya vizuri katika utendaji wao kwa mwaka 2025.

Aidha, jumuiya hiyo imejipanga kwa mwaka 2026 kuwa chombo mahususi cha kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wake.

Katika kikao hicho cha Baraza, mgeni rasmi alikuwa Diwani wa Kata ya Makuburi, Mhe. Issa Faru, ambaye alipata fursa ya kukabidhi vyeti vya pongezi kwa viongozi wa matawi waliofanya vizuri. Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Faru amesema kuwa ataendelea kushirikiana na jumuiya hiyo katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata ya Makuburi.

Katika mipango yake, jumuiya hiyo inalenga kuongeza idadi ya wanachama, kuwajengea uwezo wanawake, kuwawezesha kiuchumi, pamoja na kuendelea kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la UWT Kata ya Makuburi kilichofanyika 17 Januari, 2026 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UWT Kata hiyo, Bi. Editha Ngotanile, amesema kuwa miongoni mwa mipango ya jumuiya hiyo kwa mwaka 2026 ni kutoa msaada kwa wahitaji, kuwainua wanawake kiuchumi kupitia shughuli za ujasiriamali, pamoja na kufuatilia kwa ukaribu utendaji wa ngazi ya matawi ili kuhakikisha vikao vinafanyika mara kwa mara, kwani vikao ndiyo uhai wa jumuiya.

Bi. Ngotanile ameongeza kuwa matawi yote ndani ya jumuiya hiyo yameanzisha vikoba kwa lengo la kuwasaidia wanawake kuachana na mikopo kandamizi.

Amesema kuwa mara nyingi wanawake wamekuwa wakiingia katika mikopo hiyo bila uelewa wa kina, hali inayosababisha changamoto mbalimbali, hivyo vikoba vitakuwa msaada mkubwa kwao.

Aidha, amesema kuwa miongoni mwa mikakati ya jumuiya hiyo kwa mwaka huu ni ujenzi wa ofisi ya UWT katika ngazi ya kata, jambo litakalosaidia kurahisisha utekelezaji wa mipango na kuleta matokeo chanya kwa jumuiya.

Kwa upande wake, Katibu wa UWT Kata ya Makuburi, Bi. Severina Minga, amesema kuwa katika kikao hicho wameweka mipango mbalimbali yenye lengo la kukisaidia Chama na Serikali, ikiwemo maandalizi ya maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika Aprili 5, 2026.

Bi. Minga amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi kila mmoja kwa nafasi yake, huku akisisitiza umoja na ushirikiano kuwa ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya jumuiya, chama na Serikali kwa ujumla.

Nao wajumbe wa Halmashauri Kuu ya UWT Kata ya Makuburi, Bi. Hilda Luhombo na Bi. Asinath Jamson, wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa uongozi ili kuhakikisha mipango yote iliyopangwa inatekelezwa kwa kiwango kikubwa na kuleta tija ndani ya jumuiya.