Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Mkutano wa Sita
Jukwaa la Uongozi la Afrika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulujijini Dar es salaam leo Agosti 20, 2019
RAIS Dk. John Magufuli, ametaja mambo sita zinazoifanya Afrika iendelee kuwa maskini na kutawaliwa na wakoloni mbali ya utawala wa kikoloni kukoma miaka zaidi ya 50 iliyopita.
Alisema hayo jana ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wa sita wa jukwaa la viongozi barani Afrika (6th African Leadership Forum), ambapo ulikutanisha maraisa sita wastaafu wa Afrika kujadili masuala mbalimbali yanayoifanya Afrika kubaki nyuma.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: Kukuza Usimamizi mzuri wa Rasilimali za Asili kwa Mabadiliko ya Kijamii na kiuchumi barani Afrika, ambapo kikubwa ni kuangalia namna viongozi wanavyosimamia rasilimali za asili kwa ajili ya mabadiliko ya kiuchumi barani Afrika.
Akitaja sababu hizo Rais Magufuli alisema, kwanza ni kuwepo na masalia ya fikra za ukoloni. Kuhusu sababu hii alibainisha bado kuna viongozi wa kiafrika wanafikiria kutawaliwa badala ya kujitawala.
“Kama hujitegemei huwezi kuwa huru, watu waliotutawala hawawezi kuwa wasaidizi wetu, lazima tuondokane na fikra za kikoloni tuanze kujiamini kama tunaweza kama waafrika, tukisimama pamoja naamini tutafanya makubwa,” alisema Rais Magufuli.
Sababu ya pili alisema ni kushindwa kusimamia rasilimali za Afrika, ambapo katika hili alisema wengi wanaamini fedha ndio msingi wa maendeleo kitu ambacho si kweli.
“Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutaja sababu tatu za kuendelea, alisema ili tuendelee lazima tuwe na watu, siasa safi na uongozi bora. Hakutaja mahali popote kama fedha ni msingi wa maendeleo.
“Akili zetu tumezielekeza kwenye mikopo na misaada, hakuna mjomba kutoka nje atakayekuja kutusaidia, tunazo rasilimali zalima tuzitumie vizuri halafu pesa zenyewe zitakuja,” alisema.
Aidha, sababu ya tatu ya kuifanya Afrika ibaki kuwa masikini Rais Magufuli alisema ni ukosefu wa ubunifu katika masuala ya tekonolojia na uanzishwaji viwanda.
Alibainisha, malighafi nyingi za bidhaa zinazouzwa katika soko la dunia zinatoka barani Afrika, lakini viongozi wamekosa uthubutu katika ubunifu na teknolojia ya viwanda.
Sababu ya nne ni migogoro na hali tete ya kisiasa barani Afrika, ambapo watu wanatumia muda mwingi kufanya siasa badala ya shughuli za kimaendeleo. Matokeo yake kunakuwa na vurugu zinazorudisha nyuma shughuli za kimaendeleo.
“Maeneo mengi yenye rasilimali kuna migogoro, tunafahamu migogoro hii inaanzishwa na mabeberu kwa kushirikiana na vibaraka wao waliopo barani Afrika. Wakati nchi zipo kwenye vurugu wao wanavuna rasilimali zetu wanatuachia mashimo,” alisema.
Sababu ya tano aliitaja ni mikataba mibovu inayosababisha kuchukuliwa kwa rasilimali za Afrika. Ambapo, viongozi wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na mabeberu kuchota rasilimali za Afrika kwa kutumia mikataba isiyozingatia pande mbili za makubaliano.
“Mikataba mingi ilikuwa inasimamia upande mmoja, mmoja ananufaika na mwingine anaumia. Hii yote imesababishwa na ukosefu wa uzalendo, mabebertu na vibaraka wao wanawahadaa wananchi na kuchukua rasilimali zao, wao wanaangalia matumbo yao lakini wanaoumia na vizazi vijavyo,” alibainisha.
Katika mlolongo wake, Rais Magufuli aliitaja sababu ya tano kuwa ni uharibifgu wa mazingira na maliasili zilizopo barani Afrika ambazo hazipatikani kwengineko.
Alisisitiza, uharibifu wa mazingira unaofanyika kwa kukata miti hovyo ili kuitumia kwa nishati ya mkaa kunasababisha ukame, mafuriko na mmommonyoko wa ardhi.
“Yote hii inasababishwa na ukosefu wa nishati ya uhakika ya kutumia majumbani, lakini tumeamua kuondoa tatizo hili kwa kushirikiana kwa pamoja kama nchi za Kiafrika ili kuacha utegemezi,” alisema Rais Magufuli.