NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Timu ya Taifa ya Senegal imerejeshewa rasmi ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kutengua uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliokuwa umeipokonya taji hilo na kulikabidhi kwa Morocco.
Uamuzi huo umetolewa leo, Novemba 24, 2026, kufuatia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Senegal (FSF), kupinga uamuzi wa CAF uliotangaza Morocco kuwa mabingwa kwa ushindi wa mezani wa mabao 3-0.
Senegal ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Morocco bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Januari 18, 2026, jijini Rabat, Morocco. Bao pekee la ushindi lilifungwa na kiungo Pape Gueye katika dakika za nyongeza.
Hata hivyo, mchezo huo uliingia kwenye utata baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani kwa takribani dakika 15 wakipinga uamuzi wa mwamuzi wa kutoa penalti kwa Morocco dakika za mwisho za mchezo. Penalti hiyo iliyopigwa na Brahim Diaz iliokolewa, kabla ya mchezo kuendelea na Senegal kupata ushindi.
Machi 17, 2026, Kamati ya Rufaa ya CAF ilibatilisha matokeo ya uwanjani na kuitangaza Senegal kuwa imepoteza mchezo huo kwa mujibu wa kanuni za mashindano, huku Morocco ikipewa ushindi wa mabao 3-0 na kutangazwa mabingwa. Uamuzi huo uliifanya Senegal kuwasilisha rufaa CAS, ambayo sasa imerejesha matokeo ya awali ya fainali na kuithibitisha Senegal ndiyo mabingwa rasmi, na hakuna chombo kingine cha juu cha kukata rufaa zaidi ya CAS.
