Na Baltazar Mashaka, Ilemela

Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imewataka wakulima wa pamba nchini kuzingatia kanuni bora za kilimo pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji, ubora wa pamba na kipato chao.

Ofisa Kilimo wa TCB Wilaya ya Sengerema, Salmath Kisongo, alisema matumizi ya teknolojia za kisasa yamekuwa mkombozi kwa wakulima, hususan wenye mashamba makubwa, kwa kurahisisha maandalizi ya mashamba na shughuli nyingine za kilimo, hatua inayoongeza tija ya uzalishaji.

Kisongo alitoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na wananchi waliotembelea banda la TCB katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza.

Alisema zao la pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini kwani linachangia kati ya asilimia 10 hadi 20 ya mapato ya fedha za kigeni, huku likiwaajiri takribani asilimia 40 ya Watanzania waliopo katika mnyororo wa thamani wa zao hilo. Aidha, pamba ni chanzo muhimu cha malighafi kwa viwanda vya nguo na bidhaa nyingine zinazotokana na nyuzi.

“Asilimia 98 ya pamba nchini huzalishwa katika mikoa 12 ya Kanda ya Magharibi, huku Kanda ya Mashariki ikichangia chini ya asilimia mbili. Ili kuongeza tija na ubora wa zao hili, wakulima wanapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha pamba,” alisema Kisongo.

Alifafanua kuwa TCB, kupitia maofisa ugani, inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kanuni 10 za kilimo bora cha pamba. Kanuni hizo ni pamoja na kuandaa shamba kwa wakati, kupanda mapema na kwa mstari kwa kuzingatia nafasi sahihi, kupunguza miche, kufanya palizi kwa wakati, kutumia mbolea za asili ikiwemo samadi na mboji pamoja na virutubisho vinavyohitajika ili kuongeza uzalishaji.

Kisongo alisema maonesho ya Nane Nane yamekuwa fursa muhimu ya kuelimisha wananchi, ambapo wakulima na wanafunzi wa shule za sekondari wanaotembelea banda la TCB wamepatiwa elimu kuhusu uzalishaji wa pamba kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji, utunzaji, uvunaji, matumizi ya teknolojia za kisasa na mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia kama matrekta na ndege zisizo na rubani (dron) kwa ajili ya kupulizia viuatilifu yamepunguza muda na gharama za uzalishaji, hasa kwa wakulima wenye mashamba makubwa, na hivyo kuongeza ufanisi na ubora wa zao la pamba.