Na Scolastica Sambi – MAELEZO
Tanzania imeendelea kuthibitisha mafanikio yake katika tasnia ya mbegu baada ya kushika nafasi ya tatu kati ya nchi 55 za Afrika kwa ubora wa sekta ya mbegu, mafanikio yanayotokana na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika utafiti, uzalishaji na uthibiti wa ubora wa mbegu.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 07, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimagu, amesema kuwa Tanzania imepata alama 7.25 kati ya 10 katika tathmini ya The African Seed Access Index (TASAI 2023), ikitanguliwa na Afrika Kusini na Zambia pekee.
“Tanzania inashika nafasi ya tatu kati ya nchi 55 za Umoja wa Afrika kwa ubora wa sekta ya mbegu. Mafanikio haya yanatokana na uwekezaji wa Serikali katika utafiti, uthibiti wa ubora wa mbegu na kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa mbegu bora,” amesema Chimagu.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa bajeti ya tasnia ya mbegu kutoka shilingi bilioni 16.79 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 85.15 mwaka 2025/26, fedha zilizowezesha kuboresha utafiti, uzalishaji wa mbegu bora na huduma za uthibiti wa ubora zinazotolewa na TOSCI.
Aidha, uzalishaji wa mbegu zilizothibitishwa ubora umeongezeka kutoka tani 50,750 mwaka 2021/22 hadi tani 78,842 mwaka 2025/26, huku zaidi ya asilimia 57 ya mbegu hizo zikizalishwa nchini kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kampuni binafsi, hatua iliyopunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.
Aidha, amesema kuwa Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 7.2 katika ujenzi na ukarabati wa maabara za kisasa za mbegu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa, hatua itakayoongeza uwezo wa Tanzania kutoa huduma za upimaji wa mbegu kwa viwango vya kimataifa.
TOSCI imeendelea kudumisha ithibati ya kimataifa ya International Seed Testing Association (ISTA) na uanachama wa skimu za mbegu za OECD, jambo linalorahisisha mbegu zinazozalishwa nchini kukubalika katika masoko ya kimataifa na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta ya mbegu.
Huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora, matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula barani Afrika na duniani kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
