Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, amesema ushiriki wa wanawake katika sekta ya ushirika una mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa familia, jamii na taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha kupata fursa zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.Akizungumza Agosti 06,2026 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Wanawake katika Sekta ya Ushirika lililoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), sambamba na Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mpanju amesema Kuwa  maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila ushiriki wa wanawake.

Aidha, amesema Kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira bora yatakayowapa wanawake nafasi sawa ya kumiliki rasilimali, kupata mitaji, masoko, teknolojia na elimu, hatua ambazo zitasaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Maendeleo hayawezi kuwa kamili wala endelevu kama wanawake wataachwa nyuma. Taifa lolote linalowekeza kwa wanawake huwekeza katika ustawi wa familia, jamii na taifa kwa ujumla,” amesema Mpanju.

Aidha, amebainisha kuwa sekta ya ushirika ina nafasi muhimu katika kuwawezesha wanawake kuongeza kipato kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji na biashara, huku akihimiza ushiriki wao katika nafasi za maamuzi ndani ya vyama vya ushirika.

Kwa upande wake, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema Jukwaa la Wanawake wa Ushirika Tanzania linalenga kujenga uwezo wa wanawake wanachama wa ushirika, kuongeza ushiriki wao katika uongozi na maamuzi, pamoja na kuwawezesha kutumia fursa za ujasiriamali, masoko, teknolojia na uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya sekta ya ushirika.

Amesema jukwaa hilo linatarajiwa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa vyama vya ushirika, kuimarisha uwezo wao wa kusimamia shughuli za kiuchumi kwa tija na kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili wanawake na vijana wapate mafunzo, mitaji, masoko na fursa za uwekezaji.Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake la Taifa, Pili Marwa, amesema Kuwa  jukwaa hilo limewakutanisha wanawake 460 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mtandao wa ushirikiano katika maeneo ya mitaji, mikopo na masoko ya mazao ndani na nje ya nchi.

Naye Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Paulina Maingo, amesema Jukwaa la Wanawake wa Ushirika Tanzania litawawezesha wanawake na wadau wa ushirika kujadili masuala ya maendeleo ya sekta hiyo nchini. Ameongeza kuwa jukwaa hilo litahamasisha wanawake kujiunga na vyama vya ushirika ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, amebainisha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vinawanyima kujiamini na kuwazuia kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Amesema elimu ya ushirika kupitia mafunzo na uhamasishaji itasaidia wananchi kutambua manufaa ya kujiunga na vyama vya ushirika.

Jukwaa hilo limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Ushirika kwa Maendeleo Jumuishi: Usimwache Mwanamke Nyuma,”