Mwamvua Mwinyi, Pwani
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 206 kwa makosa mbalimbali ya jinai katika operesheni na misako iliyofanyika kati ya Juni na Julai mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, akizungumza na waandishi wa habari alisema, kati ya waliokamatwa, watuhumiwa 89 walihusishwa na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
“Polisi walikamata puli 59 za bangi, kete 2,361, misokoto sita, pakiti 150 za bangi zenye uzito wa kilo 2.8, pamoja na bunda 95 za mirungi zenye uzito wa kilo 95 zilizokuwa zinasafirishwa kwa pikipiki mbili.”
Aidha, watu 35 walikamatwa wakitengeneza na kusambaza pombe haramu ya moshi, huku lita 172 za pombe hiyo na mitambo minne ya kutengenezea zikikamatwa.
Katika mapambano dhidi ya magendo, watuhumiwa tisa walikamatwa wakiingiza nchini mafuta ya kula yenye ujazo wa lita 1,520 kupitia bandari bubu za Wilaya ya Bagamoyo wakilenga kukwepa ushuru wa Serikali.
Morcase alieleza pia wamefanikiwa kuokoa mali mbalimbali zilizoibwa zikiwemo pikipiki 54, betri za magari 83, televisheni mbili, katoni 227 za maji, nyaya za shaba kilo 203, mifuko 20 ya saruji, maboksi 27 ya tiles pamoja na vifaa vingine.
Kwa upande wa usalama barabarani, madereva wanane walifungiwa leseni, huku madereva 71 wakifikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.
Vilevile alibainisha, makosa 20,380 ya barabarani yalibainika na wahusika kutozwa faini pamoja na kupewa elimu ya usalama barabarani.
Morcase alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
