Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Miss World Tanzania 2026, Latricia Ian Sawe, ameagwa rasmi leo kuelekea nchini Vietnam kuiwakilisha Tanzania katika Tamasha la 73 la Miss World litakalofanyika kuanzia Agosti 9 hadi Septemba 5, 2026, huku fainali zikitarajiwa kufanyika Septemba 5 katika Jiji la Ho Chi Minh.
Latricia anakuwa mwakilishi wa 30 wa Tanzania kushiriki katika mashindano ya Miss World tangu nchi ilipoanza kushiriki katika jukwaa hilo la kimataifa, hatua inayodhihirisha kurejea kwa Tanzania katika mashindano hayo baada ya kipindi cha kutoshiriki.
Katika hafla ya kumuaga, Latricia alikabidhiwa Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni ishara ya heshima, imani na wajibu wa kuiwakilisha nchi mbele ya dunia.
Ushiriki wa mwaka huu pia unaweka historia mpya kwani ni mara ya kwanza mashindano ya Miss World Tanzania kuandaliwa na 361 Degrees Africa Limited, chini ya uongozi wa Mbunifu maarufu wa mitindo nchini na Mkurugenzi wa Taifa wa Miss World Tanzania, Mustafa Hassanali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Hassanali amesema kuiwakilisha Tanzania katika fainali za Miss World ni heshima kubwa na wajibu mzito, akieleza kuwa Latricia ameandaliwa kikamilifu kuwa balozi wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.
“Tuna imani mwakilishi wetu ataonesha maadili ya uadilifu, huruma na ubora huku akitangaza utamaduni wetu na kuonyesha uwezo wa wanawake wa Kitanzania. Tunawaomba Watanzania wote waungane kumuunga mkono katika safari yake,” amesema Hassanali.
Kwa upande wake, Latricia amesema anajivunia kupewa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania na kwamba amebeba ndoto, matumaini na matarajio ya Watanzania wote.
Amesema ataitangaza Tanzania kwa heshima kupitia utamaduni wake, vivutio vya utalii na mradi wake wa Nuru ya Elimu unaotekelezwa chini ya programu ya kimataifa ya Beauty With a Purpose, unaolenga kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Nimebeba si tu bendera ya Taifa bali pia ndoto na nguvu za kila Mtanzania. Nitajitahidi kuiwakilisha nchi yangu kwa heshima, uhalisia na dhamira ya kuleta mabadiliko kupitia mradi wa Nuru ya Elimu,” amesema Latricia.
Waandaaji wa Miss World Tanzania wamesema kupitia uongozi mpya wanakusudia kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa kwa kuwawezesha wanawake vijana kupitia uongozi, utetezi wa masuala ya kijamii, kubadilishana tamaduni na programu ya Beauty With a Purpose.
Aidha, wamewashukuru wadhamini na washirika mbalimbali waliofanikisha maandalizi ya safari ya Latricia, wakiwemo ITV, Radio One, Rush Trek Tours, Whitesands, Wix Product, Zen Spa, Atsoko, Tanzanite Gin, Infocus, Assemble Insurance, Timelapse, AR Fitness, Kiwango Security, Alko Vintage na Nexia Tanzania.
Pia wamewatambua wabunifu wa mitindo wa Tanzania waliobuni mavazi yatakayotumika kutangaza ubunifu, utamaduni na utambulisho wa Tanzania katika mashindano hayo, wakisema mchango wao ni sehemu muhimu ya kuipeperusha vyema bendera ya Taifa.
Kwa upande mwingine, waandaaji wamezipongeza taasisi zinazoshirikiana katika mradi wa Nuru ya Elimu, zikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Doris Mollel Foundation, Enable Youth Foundation na Mustafa Hassanali Foundation kwa mchango wao katika kusaidia watoto wenye tawahudi na changamoto nyingine za maendeleo.
Latricia sasa anatarajiwa kuanza safari yake ya mashindano nchini Vietnam akiwa na dhamira ya kuitangaza Tanzania kupitia uzuri wake, utamaduni, utalii na miradi ya kijamii, huku Watanzania wakihimizwa kumuunga mkono katika harakati zake za kuwania taji la 73 la Miss World.

