Na John Walter-Babati

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb), akiendelea na ziara maalum ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika mkoa wa Manyara Halmashauri ya Mji wa Babati na Babati Wilaya amefanya mkutano na wananchi na kusisitiza watendaji kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji na uzalendo ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Katika ziara hiyo, ametembelea na kuzindua Jengo la Utawala la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), kukagua ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi Babati pamoja na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mrara kwa kiwango cha lami na boksi kalavati.

Akizungumza na wananchi, Mhe. Aweso amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku akiwataka watumishi kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa. “Kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa wakati, kwani dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi kwa ufanisi,” alisema.

Katika ukaguzi wa miradi ya miundombinu, Waziri Aweso ameeleza kuwa ujenzi wa barabara una mchango mkubwa katika kuchochea uchumi wa wananchi, hususan barabara inayoelekea lango la Hifadhi ya Tarangire ambayo itaongeza fursa za biashara, uwekezaji na utalii. Aidha, aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Kwa upande wa huduma ya maji, Mhe. Aweso alisisitiza kuwa maeneo yote yenye changamoto ya upatikanaji wa maji yapatiwe ufumbuzi wa haraka ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu bila kuchelewa ambapo pia amewataka viongozi na wataalamu wa sekta mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili fedha zinazotolewa na Serikali ziendelee kuleta manufaa ya kudumu kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla.

Katika mkutano huu wa hadhara Waziri Aweso ameungana pamoja na Mhe Daniel Baran Sillo mbunge wa jimbo la Babati Vijijini na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .