Mbegu za wakulima zinazochangia zaidi ya asilimia 60 ya mbegu zinazotumiwa nchini bado hazina utaratibu rasmi wa kuhakikisha ubora wake, hali inayozuia kutambuliwa rasmi na kupunguza fursa za wakulima kunufaika na rasilimali hizo.
Hayo yameelezwa leo Agosti 5, 2026 jijini Dodoma na Mratibu wa Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), wakati wa mjadala kuhusu utambuzi wa mifumo ya mbegu zinazosimamiwa na wakulima na mchango wake katika mifumo endelevu ya chakula. Amesema tofauti na mbegu zilizothibitishwa, mbegu za wakulima bado hazitambuliwi moja kwa moja chini ya mfumo wa sasa wa sheria, jambo linalozuia kuwepo kwa utaratibu wa kuzihakiki, kuzisimamia na kuzilinda kisheria.
Amesema Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 pamoja na marekebisho yake na Kanuni za mwaka 2017 zimejikita zaidi katika mbegu zilizothibitishwa, huku mbegu za wakulima zikiendelea kukosa nafasi katika mfumo rasmi wa usimamizi wa mbegu nchini.
Katika mjadala huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimagu, amesema Serikali imeanza hatua za kusajili baadhi ya mbegu za asili ili kuzitambua rasmi na kuweka mfumo wa kuzisimamia.
Amesema ongezeko la watu, upanuzi wa miji na mabadiliko ya matumizi ya ardhi vimechangia kupotea kwa aina mbalimbali za mimea na mbegu za asili, hivyo kuna umuhimu wa kuchukua hatua za haraka za kuzihifadhi.
“Mbegu bora lazima ziwe na ubora wa kijenetiki, ziwe salama dhidi ya magonjwa na ziweze kutoa mavuno yanayokidhi matarajio ya wakulima. Usimamizi wa mbegu unalenga kulinda wakulima dhidi ya bidhaa zisizo na ubora,” amesema Chimagu.
Ameongeza kuwa usajili wa mbegu za asili utarahisisha kulinda haki za wamiliki wa mbegu hizo, kuongeza fursa za biashara na kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai pamoja na usalama wa chakula nchini.
Wadau waliohudhuria mjadala huo wameitaka Serikali kukamilisha mfumo wa uhakiki na usimamizi wa ubora wa mbegu za wakulima ili ziingizwe rasmi katika mfumo wa usimamizi wa mbegu nchini, huku wakisisitiza umuhimu wa kulinda haki za wakulima wanaohifadhi, kubadilishana na kuendeleza mbegu za asili kwa vizazi vingi.
Aidha, wataalamu wa kilimo wameeleza kuwa mbegu za asili zina uwezo mkubwa wa kustahimili ukame na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi, hivyo zina mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo ya kilimo endelevu nchini.

