Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa elimu kwa jamii ya Ngorongoro kuhusu mfuko wa Ngorongoro Scholarship Fund unaolenga kuwezesha wanafunzi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kupata fursa ya masomo ya elimu ya juu kupitia ufadhili Ngorongoro Fund.
Elimu hiyo iliyotolewa katika ofisi za Ngorongoro ilijumuisha wadau muhimu wanaoguswa na mpango huo ambao ni viongozi wa jamii, wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali ambao wamepewa uelewa kuhusu vigezo vya mkopo, sifa za waombaji pamoja na kupitia na kujadili mwongozo wa programu ya Ngorongoro Scholarship Fund.
Katika kikao hicho, viongozi wa jamii wamepongeza hatua ya Mamlaka ya kushirikiana na HESLB katika kuandaa na kuboresha mwongozo wa mfuko huo, wakieleza kuwa utasaidia kuweka utaratibu unaozingatia usawa, uwazi na mahitaji ya wakati katika kuwawezesha wanafunzi wenyeji kupata fursa za elimu ya juu.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro, Mhe. Edward Maura, aliipongeza Mamlaka ya Ngorongoro na HESLB kwa kutoa elimu kuhusu Ngorongoro Scholarship Fund hasa jinsi wanufaika wanavyoweza kutambua fursa, kujaza fomu na kufuata taratibu za kuomba ufadhili.
“Tunawapongeza Ngorongoro na Bodi ya Mikopo kwa kutoa elimu hii kwa jamii na wanafunzi na kusaidia kuwaondolea wanafunzi changamoto na uelewa mdogo wa namna ya kuomba na kupata mikopo huu, tunaamini maamuzi haya ya Serikali yanalenga kuimarisha mahusiano kati ya jamii na Ngorongoro na tunaamini wanafunzi na jamii watatumia fursa zinazotolewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa” alisema Mh. Maura.
Utekelezaji wa program hii unalenga kuimarisha ushirikiano na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wa Ngorongoro ambapo elimu wanayopata itasaidia ushiriki wao katika program za uhifadhi endelevu na kuvutia wageni kupitia vivutio vya utalii vilivyopo.

