Wananchi wanatarajiwa kunufaika na mfumo mpya wa mita za maji za malipo kabla ya matumizi (prepaid meters) nchini, hatua inayolenga kuondoa malalamiko ya bili kubwa za maji na kuwapa watumiaji uwezo wa kudhibiti matumizi yao kulingana na fedha wanazolipia.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Afisa Uhusiano na Masoko wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Haji Athumani Msovu, amesema mfumo huo unafanya kazi kwa utaratibu unaofanana na mita za umeme za malipo kabla ya matumizi, ambapo mtumiaji hulipia huduma kabla ya kutumia maji.

Amesema teknolojia hiyo itasaidia kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma za maji kwa kuwa kila mtumiaji atatumia kiwango cha maji kinacholingana na fedha alizolipia.

Msovu amesema mita hizo tayari zimeshaanza kufungwa kwenye Vyombo vya utaoaji huduma ya maji ngazi ya jamaii (CBWSO) katika mikoa mbalimbali huku mrejesho kutoka kwa wananchi ukiwa wa kuridhisha.

Aidha, amesema RUWASA imeingia mkataba na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kwa ajili ya kutengeneza mita hizo na baada ya kufanya majaribio mita hizo zikaonekana kuwa na ufanisi zaidi ambazo zimaanza kusambazwa kwa mikoa mbalimbali ambayo RUWASA inahudumia.

RUWASA ikaichagua ATC na kuingia nayo makubaliano ili Vyombo vya utaoaji huduma ya maji ngazi ya jamaii (CBWSO) na Mamlaka za Maji zinayohitaji ziweze kuagiza moja kwa moja kutoka chuo kuagiza kulingana na uwezo wao wa kifedha na mahitaji

Msovu ameongeza kuwa mita hizo zimetengenezwa kwa plastiki maalumu inayostahimili kutu, hivyo zinafaa hata katika maeneo yenye maji ya chumvi na zitasaidia kupunguza hitilafu pamoja na gharama za matengenezo.

Amesema RUWASA itaendelea kukusanya maoni kwa wananchi ili kuendelea kuuboresha kwa nia kuhakikisha unakutumika kwa ufanisi mkubwa katika maeneo yote zitakapofungwa mita hizo nchini.