Mfuko wa SELF (SELF MF) umezitaka wananchi, hususan wakulima na vijana, kutumia fursa za mikopo nafuu zinazotolewa na taasisi hiyo ili kuwekeza katika shughuli za kilimo, kuongeza thamani ya mazao na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja wa Soko na Uhamasishaji wa SELF MF, Linda Mshana, amesema taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Fedha imejikita katika kutoa huduma za kifedha zenye masharti nafuu kwa wananchi, huku sekta ya kilimo ikiwa miongoni mwa maeneo yenye kipaumbele.

Mshana amesema SELF MF inatoa mikopo inayogusa mnyororo mzima wa thamani wa kilimo kuanzia uzalishaji, uchakataji, usafirishaji, kuongeza thamani ya mazao hadi bidhaa kumfikia mlaji.

“Tumekuja kuwaonyesha wananchi kuwa kuna fursa nyingi za mikopo katika sekta ya kilimo. Tunafadhili shughuli zote katika mnyororo wa thamani wa kilimo ili kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kukuza biashara zao,” amesema Mshana.

Amesema taasisi hiyo pia inatumia maonesho hayo kuhamasisha vijana kujiajiri kupitia ubunifu katika kilimo, akitolea mfano mjasiriamali wa Mobile Coffee Shop ambaye ameanzisha biashara ya kusindika na kuuza kahawa kupitia duka linalohama kulingana na mahitaji ya wateja.

“Vijana wanaweza kuiga ubunifu huu hata kwenye mazao mengine kwa kuanzisha biashara za kutembea za vyakula, nafaka au bidhaa nyingine za kilimo. Kinachohitajika ni ubunifu na kujifunza,” amesema.

Aidha, amesema SELF MF imewaleta wadau mbalimbali wanaoonyesha teknolojia rafiki kwa mazingira, ikiwemo majiko yanayotumia umeme mdogo na teknolojia zinazosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, hatua inayochangia uhifadhi wa mazingira na kuimarisha uzalishaji wa kilimo.

Mshana amesema wananchi pia wanapata elimu kuhusu bima za mazao, akieleza kuwa huduma hiyo huwasaidia wakulima na wafanyabiashara kujikinga dhidi ya hasara zinazoweza kutokea wakati wa usafirishaji au uhifadhi wa mazao.

“Tunawahamasisha wananchi kutumia bima za mazao kwa sababu zinaweza kuwasaidia kurejea katika hali yao ya awali endapo watapata hasara wakati wa biashara,” amesema.

Ameongeza kuwa SELF MF tayari imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 400 kwa wanufaika wapatao 450,000, huku karibu asilimia 40 ya mikopo yote ikielekezwa kwenye sekta ya kilimo.

Mshana amewakaribisha wananchi kutembelea banda la SELF MF katika Maonesho ya Nanenane yaliyopo ndani ya hema la Wizara ya Fedha katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma, pamoja na mabanda ya taasisi hiyo yaliyopo katika maonesho ya Nanenane mikoa ya Morogoro, Lindi na Mwanza.

Amesema SELF MF pia ina matawi katika mikoa 12 nchini yanayohudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali na kuwahimiza Watanzania kufika kupata ushauri na huduma za mikopo zitakazowawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.