Mchambuzi Mwandamizi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Bw. Doto Namkaa akitoa maelezo kwa Dkt. Wilfred Mbowe Mkurugenzi Tawi la Benki Kuu ya Tanzania, Dodoma kulia na Dkt. Francis Assenga Meneja Fedha na Utawala Tawi la Benki Kuu, Dodoma katikati wakati wapilotebelea banda la BoT katika maonyesho ya Nanenane Dodoma Agosti 03, 2026.

………..
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yameendelea kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya fedha kwa kurahisisha miamala, kuongeza usalama wa malipo na kusaidia Serikali kukusanya mapato kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza katika banda la Benki Kuu ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mchambuzi Mwandamizi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Bw. Doto Namkaa, amesema moja ya majukumu ya Benki Kuu ni kusimamia mifumo ya malipo nchini pamoja na kutoa leseni kwa watoa huduma za malipo ili kuhakikisha huduma hizo zinakuwa salama na zenye kuaminika.
Namkaa amesema BoT imefanikiwa kuunganisha mifumo ya malipo nchini kupitia teknolojia inayomwezesha mtumiaji kutumia akaunti moja kufanya miamala katika taasisi mbalimbali za kifedha bila kulazimika kufungua akaunti nyingi.
“Kupitia mifumo ya malipo ya Benki Kuu, wananchi sasa wanaweza kutumia akaunti moja kufanya malipo katika maeneo mbalimbali. Mfumo huu umeondoa changamoto ya kuwa na akaunti nyingi na umefanya huduma za kifedha zipatikane kwa urahisi zaidi,” amesema Namkaa.
Ameeleza kuwa mfumo wa Tanzania Instant Payment System (TIPS) umewezesha malipo kufanyika kwa urahisi kati ya benki na watoa huduma za fedha, ambapo mteja anaweza kutumia namba ya malipo (Lipa Namba) kufanya miamala bila kujali taasisi aliyosajiliwa.
Kwa mujibu wa Namkaa, maendeleo hayo yamewanufaisha zaidi wananchi wa vijijini na wakulima, ambao sasa wanaweza kupokea au kutuma fedha moja kwa moja kupitia simu au akaunti zao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za benki.
“Mifumo hii ipo chini ya usimamizi wa Benki Kuu, hivyo ni salama na wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi kuitumia. Huduma za fedha sasa zipo mikononi mwao kupitia simu za mkononi na benki,” amesema.
Aidha, amesema mifumo ya malipo ya BoT imegawanyika katika makundi mawili makuu ambayo ni malipo ya thamani kubwa ya zaidi ya shilingi milioni 20 na malipo ya thamani ndogo ya chini ya kiwango hicho, yote yakifanyika kwa njia za kidijitali.
Namkaa amesema matumizi ya mifumo hiyo yameongeza uwazi katika miamala na kusaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kwa urahisi zaidi kutokana na kila malipo kurekodiwa na kuelekezwa moja kwa moja kwenye akaunti husika za Serikali.
“Tunawahimiza wananchi na wafanyabiashara kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali kwa sababu inapunguza ukwepaji wa kodi, inaongeza mapato ya Serikali na kurahisisha utoaji wa huduma. Dira yetu ni kuona hata malipo mengi zaidi, ikiwemo ya huduma binafsi, yanaendelea kufanyika kupitia mifumo hii ya kisasa,” amesema Namkaa.
