DAR ES SALAAM, Tanzania – Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, atajumuika na viongozi wa kimataifa, mawaziri, watunga sera, wawekezaji, taasisi za fedha za maendeleo pamoja na viongozi wa biashara katika Mkutano wa Infra for Africa Forum 2026, unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 5 hadi 6 Agosti 2026.

Mkutano huo, ulioandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Africa50, utawakutanisha wadau muhimu kujadili mbinu bunifu za kuharakisha maendeleo na uwekezaji katika miundombinu barani Afrika, huku Mgeni Rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tarehe 5 Agosti, Rwegasira atashiriki katika mjadala wa ngazi ya juu wenye mada “Reinvesting for Expansion: Asset Recycling as a Multiplier”, akiwa pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Nishati na Miundombinu Duniani wa Standard Bank Group, Dele Kuti, na viongozi wengine waandamizi. Katika mjadala huo atazungumzia ugharamiaji wa miundombinu, uhamasishaji wa mitaji na ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuharakisha uwekezaji katika miundombinu barani Afrika.

Tarehe 6 Agosti, pia atazungumza katika kikao cha jumla chenye mada “Pace Setters: African-Designed, African-Led”, sambamba na viongozi waandamizi kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Ecobank, ATIDI na Mfuko wa Uwekezaji wa Taifa wa Angola. Kikao hicho kitachambua namna taasisi za fedha za Afrika, wawekezaji wa kitaifa, benki na wadau wa miundombinu wanavyoweza kuhamasisha mitaji ya ndani, kuimarisha mifumo ya kupunguza hatari na kuharakisha ugharamiaji wa miundombinu kupitia suluhu zinazoongozwa na Waafrika.

Stanbic Bank Tanzania inaeleza kuwa maendeleo ya miundombinu yanaendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, mtangamano wa kikanda na ustawi wa muda mrefu, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo endelevu kupitia suluhu bunifu za kifedha na ushirikiano wa kimkakati unaochochea ajenda ya maendeleo ya Tanzania na ukuaji wa Afrika.