Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho wamefanya mazungumzo na ujumbe wa Wajumbe 11 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, ulioongozwa na Mhe. Ronny Jackson, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya ya Huduma za Kijeshi ya Baraza la Wawakilishi la Marekani (House Armed Services Subcommittee).
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Julai 27, 2026 katika Ofisi za Makao Makuu ya zamani ya Jeshi la Wananchi la Tanzania, Upanga, Dar es Salaam, yalilenga kujadili maeneo ya kipaumbele katika uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, hususani ushirikiano wa biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama pamoja na hali ya amani na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Wakati wa mazungumzo hayo nchi hizo zilionyesha dhamira ya kupanua ushirikiano katika biashara na uwekezaji, hususan katika sekta za kimkakati zikiwemo gesi asilia (LNG), madini muhimu, usafiri wa anga, ulinzi na usalama. Aidha, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano baina ya wananchi wa nchi hizo mbili kwa kuondoa vikwazo vya visa kwa Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani.
Ujumbe wa Marekani uliipongeza Tanzania kwa mchango wake katika kudumisha amani na usalama wa kikanda, ikiwemo juhudi za kupambana na ugaidi na ushiriki katika operesheni za kulinda amani barani Afrika. Pande hizo mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.

