Na Happy Lazaro, Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya teknolojia ya ZOLA ELETRIC,Johnson Kiwango ambao ni wasambazaji wa teknolojia ambayo inawawezesha wauzaji wa sola kuweza kufanikiwa katika biashara zao na ni wauzaji na wasambazaji wa sola Tanzania amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi katika mbio za Redcross Maratahon Arusha zitakazofanyika agosti 2 katika.uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha .
Kiwango ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo wamekuwa miongoni mwa wafadhili katika mbio hizo.
Akizungumzia kuhusu kampuni hiyo amesema kuwa, Moja ya majukumu yao hapa Arusha ni kusambaza teknolojia ya umeme wa jua na kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.
“Tunafanya kazi ya uuzaji na usambazaji wa sola katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mtandao wa mawakala wetu, kuanzia mijini hadi vijijini, na katika sekta zote za biashara, taasisi na makazi ya wananchi.”amesema Kiwango.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila eneo lenye uhitaji wa nishati linapata suluhisho bora la umeme wa jua.”amesema .
“Tunafurahi kuwa tumekuwa na ushirikiano mzuri na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania kwa miaka mingi. “
Ameongeza kuwa ,Ushirikiano huo umewawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, hususani zinazohusu afya na ustawi wa wananchi.
“Tunaamini kuwa ni wajibu wetu kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi zinazolenga kuokoa maisha ya watu.”amesema Kiwango.
Amefafanua kuwa ,jambo muhimu ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa afya bora, ikiwemo kujitokeza kuchangia damu kwa hiari kwani hili si kwa manufaa ya wakazi wa Arusha pekee, bali kwa Watanzania wote.
“Tunawashukuru sana Redcross kwa kuendelea kutuamini na kutupa nafasi ya kushiriki katika shughuli hizi muhimu na sisi tunawaahidi kuendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika maswala mbalimbali ya kijamii.”amesema Kiwango.
“Tuna matumaini kwamba ushirikiano huu utaendelea kuimarika katika miaka ijayo ili kwa pamoja tuendelee kuwahudumia na kuwanufaisha wananchi.”
