Na.Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kuongeza upatikanaji wa mbolea nchini kwa kuagiza tani 200,000 za mbolea kwa msimu wa kilimo wa mwaka huu, sambamba na uwekezaji katika viwanda vya kuchanganya mbolea na uchakataji wa chokaa ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.
Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samuel Ahadi Mshote, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora kwa wakati, kuongeza matumizi ya pembejeo na kuimarisha usalama wa chakula pamoja na uchumi wa kilimo nchini.
Akizungumza leo Agosti 1,2026 kwenye Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Dkt.John Samuel Malecela jijini Dodoma, Mshote amesema TFC ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa mbolea zenye ubora unaokidhi mahitaji ya wakulima, huku ikijiandaa kuanza uzalishaji wa mbolea zinazochanganywa kulingana na afya ya udongo na mahitaji ya mazao mbalimbali.
Amesema katika awamu ya kwanza kampuni imeagiza tani 70,000 za mbolea, ambapo tani 35,000 za mbolea aina ya DAP tayari zimewasili nchini na zinafungashwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima kupitia utaratibu wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali.
Aidha, amesema tani nyingine 40,000 za mbolea aina ya Urea zinatarajiwa kuwasili ndani ya muda mfupi ili kuendelea kukidhi mahitaji ya msimu wa kilimo unaoanza.
“Tunataka kuhakikisha hakuna mkulima anayekosa mbolea kwa sababu ya upungufu wa usambazaji. Ndiyo maana tumejipanga kuongeza uagizaji na kuimarisha mtandao wa usambazaji nchini kote,” amesema Mshote.
Amesema TFC imepanua mtandao wake wa huduma kwa kuongeza vituo vya mauzo kutoka nane hadi 26 vilivyopo katika mikoa 22 ya Tanzania Bara, hatua iliyorahisisha wakulima kupata mbolea karibu na maeneo yao.
Mbali na vituo hivyo, kampuni hiyo inashirikiana na zaidi ya mawakala 600 wa pembejeo za kilimo, vyama vya ushirika 29 (AMCOS) pamoja na halmashauri mbalimbali ili kuhakikisha mbolea zinawafikia wakulima hadi ngazi ya vijiji.
Kwa mujibu wa Mshote, tangu TFC ilipoanza kusambaza mbolea mwaka 2022, tayari zaidi ya tani 350,000 za mbolea za ruzuku zimesambazwa kwa wakulima wanaojihusisha na uzalishaji wa mpunga, mahindi, mboga mboga, vitunguu na mazao mengine ya biashara.
Katika hatua nyingine, amesema kampuni hiyo inakamilisha ufungaji wa mtambo wa kisasa wa kuchanganya mbolea katika jiji la Dar es Salaam, ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za mbolea kwa mwaka kulingana na mahitaji ya udongo na mazao husika.
Amesema uwekezaji huo utapunguza utegemezi wa uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa mbolea maalumu kwa mazao ya kimkakati kama vitunguu, ufuta, parachichi na mazao mengine yenye thamani kubwa kiuchumi.
Sambamba na hilo,amesema TFC imeanza kutekeleza mradi wa uchimbaji na uchakataji wa chokaa mkoani Tanga baada ya kupatiwa eneo na Halmashauri ya Jiji la Tanga. Chokaa hicho kitatumika kurekebisha tindikali kwenye udongo pamoja na kuwa malighafi muhimu katika uzalishaji wa mbolea.
Mshote amesema mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea yameongeza matumizi ya pembejeo nchini kutoka tani 300,000 hadi zaidi ya tani milioni 1.2 kwa mwaka, huku takribani asilimia 80 ya wanufaika wakiwa ni wakulima wadogo.
Amesema ongezeko hilo limechangia kuimarika kwa uzalishaji wa mazao na kuiwezesha Tanzania kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 130 cha kujitosheleza kwa chakula.
Aidha, matumizi ya mbolea kwa hekta yameongezeka kutoka kilo 16 hadi kilo 24, huku Serikali na wadau wa sekta hiyo wakilenga kufikia kiwango cha kilo 30 kwa hekta kama kinavyoelekezwa na Azimio la Abuja kuhusu matumizi ya mbolea barani Afrika.
Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za umma na wananchi ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania inafikia uchumi shindani, wenye tija na jumuishi ifikapo mwaka 2050, huku akiahidi kuwa wataendelea kusimamia kwa dhati utekelezaji wa mipango na vipaumbele vilivyowekwa ili kuhakikisha maono hayo yanageuka kuwa matokeo yanayoonekana kwa manufaa ya Watanzania wote.
Mshote amewataka wakulima kutembelea banda la TFC katika Maonesho ya Nane Nane ili kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na kufahamu aina zinazofaa kwa mazao na mazingira yao, akisisitiza kuwa matumizi ya pembejeo bora ndiyo msingi wa kuongeza tija, kipato cha mkulima na ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.

