Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa wazalishaji nchini wanapaswa kuboresha ubora wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la kimataifa kila siku, badala ya kuonekana bora wakati wa maonesho pekee.
Amesema kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini zinapaswa kufikia viwango vya kimataifa ili kuongeza ushindani, kuvutia wanunuzi na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo Agosti 1, 2026, wakati akifungua rasmi Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John S. Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Aidha, amebainisha kuwa changamoto kubwa katika biashara siyo upatikanaji wa masoko pekee, bali ni ubora wa bidhaa zinazozalishwa, akisisitiza kuwa bidhaa za Tanzania zinapaswa kuwa na kiwango kinachoweza kumshawishi mnunuzi wakati wote.
Pia ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa chakula, ambapo kiwango cha utoshelevu wa chakula kimefikia asilimia 130 huku mauzo ya mazao nje ya nchi yakiongezeka kwa asilimia 77, jambo ambalo limechangia kuimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni.
Amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya kilimo, ikiwemo kutoa ruzuku ya zaidi ya tani 700,000 za mbolea zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.4.
Aidha, amesema kuwa Serikali inatarajia kuwasilisha katika mkutano ujao wa Bunge muswada wa sheria utakaofuta utaratibu wa kutaifisha mifugo inapoingia kwenye maeneo ya hifadhi, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto zinazowakabili wafugaji huku ikiendelea kulinda rasilimali za taifa.
Amebainisha kuwa Serikali itaandaa mwongozo kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuweka utaratibu mpya utakaowasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa.
Pia amesema kuwa Serikali imeendelea kuondoa baadhi ya tozo na kodi zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya sekta za kilimo na mifugo, sambamba na kuwezesha taasisi za kifedha kuongeza mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao, kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za viwandani na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Aidha, Dkt. Mwigulu amewataka maafisa ugani kuwafuata wakulima na wafugaji mashambani badala ya kusubiri ofisini ili kuwapatia elimu na teknolojia zitakazoongeza tija, huku akizitaka halmashauri kuendelea kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nanenane ili kunufaika na teknolojia mpya na fursa za masoko.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema kuwa Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na teknolojia za kilimo, huku yakishirikisha waoneshaji zaidi ya 200 na wageni kutoka mataifa 24 mwaka huu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema kuwa benki hiyo imeendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo na inalenga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.55 ndani ya miaka mitano, ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 84 ya fedha hizo tayari zimetolewa kwa wanufaika.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Ally, amesema kuwa mafanikio yanayoonekana katika sekta za kilimo na mifugo yametokana na uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau ili kuongeza tija, uwekezaji na masoko kwa ajili ya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

