Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Highridge School, Rehema Washokera, wakati akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha leo

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo , Gerald Gunza akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha
…….
Na Happy Lazaro, Arusha
Wazazi wametakiwa kuendelea kuwaunga mkono watoto wao kwa kuendeleza vipaji vyao walivyojengewa shuleni ili visiishe baada ya kuhitimu kwani nao wana wajibu mkubwa wa kuwaunga mkono kwa nafasi yao.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Highridge School, Rehema Washokera,
wakati akizungumza katika mahafali ya 17 ya darasa la saba katika shule hiyo ambapo wanafunzi hao wamepata fursa ya kuonyesha bunifu zao mbalimbali ambazo wamekuwa wakifundishwa shuleni hao.
“Mzazi asidharau kipaji cha mtoto kwa sababu elimu ya darasani pia ipo,tunahitaji mtoto awe na elimu, lakini pia aendelee kukuza kipaji chake,” amesema Rehema .
Amesema kuwa,wazazi wanaweza kuwasaidia watoto kuendeleza vipaji vyao hata wakati wa likizo, hasa pale shule wanazoenda zinapokuwa hazina programu za michezo au sanaa, akisisitiza kuwa vipaji vinaweza kuwa sehemu ya ajira na maisha ya baadaye.
Rehema amesema shule hiyo inalenga kumpa mwanafunzi elimu ya darasani pamoja na fursa za kushiriki katika shughuli mbalimbali za ziada zinazosaidia kukuza vipaji na uwezo wake.
Rehema amesema kuwa, wanafunzi hushiriki katika Arts and Crafts, pamoja na shughuli zinazohusisha teknolojia na uhandisi, ikiwa ni sehemu ya kuwapa maarifa yanayokwenda sambamba na elimu wanayopata darasani.
Rehema amesema kuwa, shule hiyo pia inaweka mkazo katika michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu na michezo mingine ya kimwili, inayolenga kusaidia wanafunzi kuwa na afya bora na kukuza uwezo wao wa kimwili.
Ameongeza kuwa shule hiyo ina vilabu mbalimbali vinavyowasaidia wanafunzi kukuza vipaji na kujiamini, ikiwemo Scouting na Debating Club, ambapo wanafunzi hujengewa uwezo wa kuzungumza mbele ya watu na kujieleza kwa ufasaha.
Amefafanua kuwa, shule hiyo ina Football Academy inayowapa wanafunzi fursa ya kukuza vipaji vyao vya soka chini ya makocha, huku ikishiriki mashindano ya Chipukizi Cup yanayofanyika kila mwisho wa mwaka.
Ameongeza kuwa, academy hiyo ina timu za watoto wa umri mbalimbali, zikiwemo Under 7, Under 9 na Under 11, huku akieleza kuwa timu ya Under 7 imekuwa miongoni mwa timu zinazofanya vizuri zaidi katika mashindano hayo.
Rehema ameongeza kuwa,pamoja na soka, shule hiyo inakuza vipaji vya wanafunzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuchora, sanaa na ubunifu wa mikono, akisisitiza kuwa shughuli hizo ni sehemu muhimu ya kuwajenga watoto kwa maisha ya baadaye.
Rehema amesema walimu wa shule hiyo wamekuwa wakisisitiza maendeleo ya mwanafunzi kwa ujumla, akieleza kuwa elimu ya darasani inapokwenda sambamba na michezo, sanaa na shughuli nyingine, humjenga mtoto kuwa na uwezo mpana zaidi wa kukabiliana na maisha.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo , Gerald Gunza, amesema shule hiyo mbali na masomo ya kawaida, ina shughuli za nje ya darasa ikiwemo klabu ya STEM inayowapa wanafunzi fursa ya kufanya ubunifu, tafiti na kuendeleza vipaji katika sayansi na teknolojia, pamoja na klabu ya sanaa inayowawezesha wanafunzi kuonyesha vipaji vya kuchora, kucheza na sanaa mbalimbali.
Gunza amesema shule hiyo imeweka mkazo mkubwa katika michezo kama sehemu ya malezi na maendeleo ya mwanafunzi, ikiwemo kushiriki mashindano mbalimbali ya michezo katika ngazi za ndani na nje ya Tanzania, jambo analosema linawasaidia wanafunzi kukuza vipaji na kujiamini.
Amefafanua kuwa,katika eneo la taaluma, imeendelea kupata matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa ya Darasa la Saba, ambapo tangu mwaka 2016 wanafunzi wake wamekuwa wakifaulu kwa asilimia 100, ambapo katika matokeo ya mwaka 2025 wanafunzi wote waliofanya mtihani walifaulu na kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Gunza amewataka wazazi kuendelea kushirikiana na shule katika malezi na elimu ya watoto wao, kwani shule hiyo inalenga kumjenga mwanafunzi kitaaluma, kiroho na katika vipaji mbalimbali, huku ikiwa na masomo ya dini kulingana na imani ya mwanafunzi.
Amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kusoma kwa bidii, kusikiliza walimu wao na kuzingatia nidhamu ndani na nje ya darasa, kwani nidhamu ni msingi muhimu wa mafanikio ya mwanafunzi katika elimu na maisha yake ya baadaye.
