Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na wananchi Ngeta, Kata ya Kikongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani tarehe 1 Agosti 2026.
Sehemu ya wananchi wa Ngeta, Kata ya Kikongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani tarehe 1 Agosti 2026 wakati wa mkutano na Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo tarehe 1 Agosti 2026.
Naibu Kamishna wa Ardhi Husein Sadick akizungumza katika mkutano kati ya wananchi wa Ngeta na Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo Agosti 1, 2026.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Bw. Abuubakar Kunenge akizungumza katika mkutano Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo tarehe 1 Agosti 2026
Na Munir Shemweta, Kibaha
Serikali imesema shauri la mgogoro wa ardhi unaowahusu baadhi ya wananchi wa Ngeta, Kata ya Kikongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, limefungwa katika ngazi ya Wizara baada ya kubainika kuwa madai yao hayana msingi wa kuendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Msimamo huo umetolewa wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, alipokutana na kuzungumza na wananchi hao kufuatia malalamiko yao ya muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi katika eneo la Makazi Mapya.
Wananchi hao wanadai kuwa walihamishwa kutoka katika maeneo yao wakati wa Operesheni Vijiji na kuacha mashamba pamoja na mazao ya kudumu, yakiwemo ya mikorosho, lakini baadaye maeneo hayo yakamilikishwa kwa watu wengine bila wao kulipwa fidia.
Wakizungumza mbele ya Waziri Akwilapo, wananchi hao wamesema wanaamini kuwa bado wanastahili kulipwa fidia kutokana na mali, mazao na maendelezo waliyoyaacha katika maeneo yao ya awali wakati walipohamishwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Serikali, Naibu Kamishna wa Ardhi nchini, Husein Sadick, amesema suala hilo katika ngazi ya wizara tayari wameandika barua kufunga mgogoro huo kutokana na sababu za kisheria pamoja na muda mrefu uliopita tangu kutokea kwa tukio hilo.
Amesema, katika mazingira hayo, Serikali haiwezi kwenda katika nyumba na maeneo yanayomilikiwa na wananchi wengine kwa sasa na kuwaelekeza walipe fidia, kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha kutotendeka kwa haki kwa watu ambao huenda walipata umiliki wao kwa kufuata taratibu.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ameeleza kuwa, msimamo wa Serikali haujatokana na upendeleo wala nia ya kumuonea mtu, bali umejengwa katika sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya ardhi nchini.
“Huo ndiyo msimamo wa Serikali na unaambatana na sheria, kanuni na taratibu zilizoainishwa vizuri katika vitabu vya sheria. Ofisi yangu haiwezi kupindisha sheria kwa lengo la kumfurahisha mtu au kundi fulani,” amesema Sadick.
Ameongeza kuwa, katika migogoro mingi ya ardhi, upande ambao hauridhishwi na uamuzi huendelea kulalamika, licha ya maamuzi hayo kutolewa kwa kuzingatia vifungu vya sheria na ushahidi uliowasilishwa.
Amesema, iwapo kila mwananchi atataka masuala ya ardhi yaamuliwe kwa matakwa yake binafsi badala ya kufuata sheria, hali hiyo inaweza kusababisha migogoro na kuvuruga utulivu katika jamii.
Amewataka wananchi kuheshimu maamuzi na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika, huku akisisitiza kuwa sheria za ardhi zinatumika kwa nchi nzima na haziwezi kubadilishwa kwa ajili ya kunufaisha kijiji, eneo au kundi moja la watu.
“Tunawaomba wananchi nao wazikubali sheria. Wasitake sheria ipindishwe ili wapate manufaa, kwa sababu sheria zilizopo ni za nchi nzima na si za kijiji kimoja,” amesema Dkt Akwilapo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema wananchi wana haki ya kukata rufaa iwapo hawajaridhika na maamuzi yaliyotolewa na mamlaka za Serikali.
Amesema wanaweza kuwasilisha malalamiko yao katika mamlaka za juu zaidi au kwenda mahakamani, lakini akawataka kuepuka kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya viongozi na watendaji waliotumia muda wao kushughulikia mgogoro huo.
Kunenge amesema Serikali ya Mkoa wa Pwani imekuwa ikifanya kazi kwa muda mrefu kujenga uaminifu na heshima kwa wananchi, hivyo si sahihi kwa watendaji wake kusingiziwa bila kuwepo ushahidi wa ukiukwaji wa sheria.
Kwa mujibu wa Serikali, Kifungu cha 15 cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114, kinaeleza hali ya haki za ardhi kwa wananchi waliohamishwa wakati wa Operesheni Vijiji, ambapo haki zao zilihamia katika maeneo mapya waliyohamishiwa.
