Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya kikao na wadau wa michezo ya kubahatisha ikiwemo waendeshaji kutoka makampuni mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala ya kodi.

Akimuwakilisha Kamishna wa Kodi za Ndani katika kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 31 Julai, 2026 Serena Hotel jijini Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Walipakodi wa Kati Bw. Godwin Barongo amesema kuwa kodi itokanayo na michezo ya kubahatisha imeendelea kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.

Bw. Barongo ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka tisa ya fedha kuanzia 2017/2018 ambapo kodi katika michezo hiyo ilianza kukusanywa hadi 2025/2026, mchango wa sekta hiyo umefikia takriban Shilingi Trilioni 1.463.

“Mchango huu mkubwa unaonesha umuhimu wa sekta hii katika kuchangia maendeleo ya taifa, na nawapongeza sana waendeshaji na wadau wote kwa ushirikiano mnaoendelea kuutoa,” amesema Bw. Barongo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Oparesheni za Kimkakati wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania Bw. Kabora Mboya ameipongeza TRA kwa kuendelea kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu katika kupata mafanikio.

Nao wadau wa sekta hiyo wamesema wapo tayari kuendelea kulipa kodi na kuiomba TRA na taasisi zingine za serikali kuendeleza utaratibu wa kukutana na wadau hao ili waweze kuimarisha ushirikiano na ufanisi wa utekelezaji wa wajibu wao