Maafisa na askari wa jeshi la Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro waliopoteza maisha, kujeruhiwa na kufanya kazi kwa uhodari wametunukiwa vyeti na fedha kutokana na kujitoa kwao kwa hali na mali kulinda rasilimali za wanyamapori na misitu.
Tuzo hizo zimetolewa tarehe 31 Julai 2026 kwenye maadhimisho ya siku ya askari wanyamapori duniani ambayo huadhimishwa kwa lengo la kuutambua mchango wa askari hao katika kulinda rasilimali za nchi na kuenzi mchango wa Askari 10 waliopoteza maisha yao na kujeruhiwa wakiwa kazini katika hifadhi ya Ngorongoro.
Naibu kamishna wa Uhifadhi huduma za shirika Aidan Makala amewapongeza askari wote wa jeshi la uhifadhi kutokana na kujitoa kwa hali na mali katika kazi hiyo huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi ili kulinda matakwa ya haki jinaii.
Naibu Kamishna Makala ameleza kuwa, askari wa uhifadhi ni nguzo ya ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu ambapo kazi hiyo haiishii kukabiliana na ujangili pekee bali inakwenda sambamba na kudhibiti uharibifu wa mazingira hususan vyanzo vya maji, ulinzi wa maisha na mali za watu dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuelimisha jamii kutunza rasilimali hizo.
Akielezea kuhusu maadhimisho ya siku ya askari wanyamapori duniani, Afisa Uhifadhi mkuu anayesimamia idara ya huduma za Ulinzi Bw. Emmaanuel Kaaya amesema kuwa Siku hiyo ilianza kuadhimishwa mwaka 2007, kwa ushirikiano baina ya Shirikisho la Kimataifa la Askari wa Wanyamapori (International Rangers Federation – IRF) na mashirika mengine ya kimataifa.
Lengo la kuanzishwa kwa maadhimisho haya ni kuutambua mchango wa Askari wa Wanyamapori na kuuenzi mchango wa Askari waliopoteza maisha wakiwa kazini. Ni siku ya kuwatambua na kuenzi mchango wa mashujaa wanaojitolea kila siku kuhakikisha hifadhi zetu zinaendelea kuwa salama kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake kamishna msaidizi mwandamizi wa Uhifadhi Gloria Bideberi amebainisha kuwa katika maadhimisho haya, Mamlaka imetoa vyeti na fedha taslimu kwa zaidi ya watumishi 30 ikiwa ni sehemu ya kuutambua mchango wao katika kazi kwa kipindi cha mwaka 2025/26.
Maadhimisho hayo yalipambwa na michezo mbalimbali iliyojumuisha mpira wa miguu, kukimbiza kuku, mazoezi ya viungo na maonesho ya kwata mbalimbali.

