Na Mwandishi wetu, Mirerani

WADAU wa madini ya Tanzanite, mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, wamechangia Sh23.6 milioni kwa ajili ya kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha ya watoto wachanga njiti.

Lengo ni kuunga mkono mkoa wa Manyara, ambao umeandaa mbio za hisani za kuchangia ujenzi wa jengo la mama na mtoto na kuboresha huduma za afya zitakazofanyika mjini Babati, Agosti 22, 2026 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.

Wadau hao wa madini ya Tanzanite, wamechangia kiasi hicho mbele ya Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga kwa nia ya kukusanya kiasi cha Sh1.6 bilioni cha kuanza ujenzi kwenye hospitali ya wilaya ya Hanang’.

Sendiga amewashukuru wadau hao wa madini ya Tanzanite kwa kuchangia fedha hizo ili kufanikisha ujenzi huo wa wodi ya watoto njiti.

“Mmefanya jambo kubwa mno kwani watoto njiti 3,000 kila mwaka kwenye mkoa wetu huwa wanazaliwa kwa hiyo tunataka tufanye jambo la baraka kwa watoto wanaozaliwa chini ya miezi tisa,” amesema RC Sendiga.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala ameeleza kwamba wadau wa madini ya Tanzanite watajitokeza kwa wingi kuunga mkono mbio hizo za kusaidia watoto njiti.

“Mimi binafsi nitakimbia kilomita tano na wana Simanjiro kwa umoja wetu tutashiriki kwa wingi mbio hizo kuchangia matibabu ya watoto wetu,” amesema Lulandala.

Mkurugenzi wa JS Magezi, William Magezi wanaochimba kitalu D extension kwa kushirikiana na Tanzanite Afrika, amesema wadau wanaochangia wanakuwa wanatoa sadaka ambayo pia inakuwa toba kwa makosa yaliyofanyika.

“Mkurugenzi mwenza wa Tanzanite Africa Will Mushi alichangia Sh2 milioni na mimi nachangia Sh2 milioni hivyo jumla tumetoa Sh4 milioni,” amesema Magezi.

Mkurugenzi wa JN Mining Justin Nyari ambaye amechangia Sh2 milioni ameeleza kuwa wadau wa nyanja tofauti washirikishwe katika sadaka hiyo.

“Hili jambo ni zuri mno katika kuokoa maisha ya watoto wetu, ushauri wangu wote wapitiwe kwa kupitia viongozi wetu wa kata na vitongoji ili kila mmoja ashiriki vile alivyojaliwa,” amesema Nyari.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa madini mkoa wa Manyara, Mokia Ole Mrefu amesema ili kuunga mkono tukio hilo, jumanne ijayo watafanya kikao na wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite ili kwa umoja wao nao wachangie.

“Pia nikiwa hapa hapa mdau wa maendeleo wa mkoa wa Manyara, Taiko Ole Kulunju, amechangia kwa kutuma Sh1 milioni na mimi binafsi nachangia Sh500,000 ili kumuunga mkono RC wetu Sendiga,” amesema Ole Mrefu.

Mmiliki mwingine wa mgodi wa madini ya Tanzanite, Joseph Manga ambaye amechangia Sh1 milioni ametoa ombi la kurekebishwa changamoto ya bei ya kibali cha kununua zana za milipuko.

“Tunakuunga mkono RC wetu kwenye hili ila tunakuomba utuangalie suala la sisi wachimbaji kulipia Sh100,000 kwa kila kibali cha kununua milipuko siyo sawa, kibali kiwe kimoja kwa bei hiyo hiyo,” amesema Manga.